Na Saulo Stephen – Singida.
Bodi ya Bima ya Amana imetoa mafunzo kwa watumishi wa Manispaa ya Singida pamoja na wanafunzi wa shule za sekondari, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kukuza uelewa wa huduma za kifedha na kuimarisha usalama wa fedha zao.
Mafunzo hayo, yametolewa Mkoani Singida
yakiwa na lengo la kuwawezesha washiriki kufahamu kwa kina majukumu ya Bodi ya Bima ya Amana na namna inavyofanya kazi katika kulinda amana za wateja wa taasisi za fedha.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo kwenye ukumbi wa Mikutano wa Manispaa ya Singida, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano wa Umma na Mawasiliano wa Bodi ya Bima ya Amana, Lwaga Mwambande, alisema ni muhimu kwa watumishi wa umma kupata elimu hiyo kwa kuwa ni miongoni mwa watumiaji wakuu wa huduma za kifedha, hivyo wanapaswa kuwa na uelewa sahihi wa mifumo ya ulinzi wa amana zao.
Kwa upande wa wanafunzi, amesema ni vyema kuanza kupata maarifa hayo mapema ili kuwajengea msingi imara wa uelewa wa masuala ya fedha, jambo litakalowawezesha kufanya maamuzi sahihi watakapofikia hatua ya kutumia taasisi za kifedha.

Aidha, bodi hiyo pia imetoa elimu kama hiyo kwa wanafunzi wa shule za Sekondari Mwenge na Mughanga, zilizopo Manispaa ya Singida lengo ikiwa ni kuwajengea uelewa wanafunzi katika shule hizo.


