BODABODA MUSOMA WAILALAMIKIA LATRA.

Na Adam Msafiri – Musoma, Mara

Baadhi ya maafisa usafirishaji maarufu kama Bodaboda katika Manispaa ya Musoma, mkoani Mara, wameilalamikia Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi katika kuwakamata bila kupewa elimu ya kutosha kuhusu matakwa ya kisheria. Wameitaka mamlaka hiyo kuongeza juhudi za kutoa elimu badala ya kuwatia hofu na kuwatoza faini kubwa.

“Juzi kulikuwa na zoezi la ukamataji maeneo ya Nyasho, ambapo maafisa waliokuja walikuwa ni mgambo wakiwa na pingu, jambo lililosababisha taharuki. LATRA inapaswa kutuelimisha kwenye vijiwe vyetu kuhusu taratibu zao, lakini badala yake wanakuja kutukamata na kututishia,” alisema Yohana Ibrahim, mmoja wa waendesha bodaboda.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa kijiwe cha bodaboda cha Nyamatare Sokoni, Yohana Masano, amesema:
“Kiwango cha kisheria cha leseni ya usafirishaji kutoka LATRA ni shilingi 17,000, lakini ukikamatwa bila kuwa nayo unatozwa faini ya shilingi 25,000. Jumla yake inafika 42,000, ambayo ni kubwa kwa sisi wanyonge. Tunaomba faini hiyo ipunguzwe.”

Akizungumzia malalamiko hayo, Afisa Mfawidhi wa LATRA mkoa wa Mara, George Robert, amesema kuwa mamlaka hiyo imekuwa ikitoa elimu mara kwa mara kwa waendesha bodaboda na wadau wengine kuhusu umuhimu wa kuwa na leseni ya usafirishaji kabla ya kuanza kutoa huduma. Alisisitiza kuwa kwa sasa LATRA inaendelea na usimamizi madhubuti kuhakikisha sheria zote zinazowasimamia wasafirishaji zinatekelezwa ipasavyo.

Kwa upande mwingine, Jeshi la Polisi Wilaya ya Musoma limewaonya waendesha bodaboda kutojihusisha na vitendo vya kihalifu kama vile usafirishaji wa mali za wizi, ubakaji, ulawiti na uhalifu mwingine wowote. Mkuu wa Polisi wa Wilaya hiyo, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi Edson Mwamafupa, amewataka waendesha bodaboda kuwa watii wa sheria bila shuruti.

“Kuwa afisa usafirishaji ni kazi halali ya kuingiza kipato. Achaneni na tabia ya kutumia pikipiki zenu kwa njia zisizo halali. Kama hufanyi kazi siku fulani, ni bora ukaweka pikipiki nyumbani kuliko kumpa mtu mwingine ambaye anaweza kuitumia kufanya uhalifu, kwani tukikamata chombo chako kwa kosa hilo, tutaanza na wewe,” ameonya Mwamafupa.

Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Mhe. Juma Chikoka, ambaye pia ni mlezi wa waendesha bodaboda wilayani humo, amewahakikishia kuwa serikali itashughulikia changamoto zao. Aliwataka bodaboda kuwa mabalozi wa amani, wazalendo, na walinzi wa utulivu hasa katika kipindi hiki ambacho taifa linaelekea kwenye uchaguzi mkuu.

Kauli hizo zimetolewa katika mkutano mkuu wa Umoja wa Waendesha Pikipiki za Abiria (Bodaboda) uliofanyika Mei 21, 2025, ambao uliwakutanisha wadau mbalimbali wa usafirishaji wilayani Musoma. Mkutano huo pia ulikuwa na lengo la kufanya uchaguzi wa viongozi wapya wa umoja huo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *