Kiongozi wa upinzani nchini Uganda, Robert Kyagulanyi maarufu Bobi Wine amedaiwa kupigwa risasi na kupata jeraha la mguuni kufuatia mzozano na maofisa wa usalama katika eneo la mji mkuu wa Kampala.
Picha zinazosambaa mitandaoni zinamwonyesha Bobi Wine akiwa amelazwa katika hospitali ya Nsambya leo Jumanne Septemba 3, 2024 akiwa na jeraha mguu kwenye wake wa kushoto.
Msemaji wa Polisi Uganda, Kituuma Rusoke amekanusha tuhuma za Bobi Wine kupigwa risasi na kusema kuwa alijikwaa wakati anaingia kwenye gari yake na kusababisha jeraha.
Maofisa wa polisi kwenye eneo la tukio wanadai kuwa (Bobi Wine) alijikwaa wakati akiingia kwenye gari lake na kusababisha jeraha, huku Bobi Wine na timu yake wakidai kuwa alipigwa risasi.
Aidha polisi nchini Uganda walisema maafisa walijaribu kumzuia Wine na timu yake kuandamana barabarani, na kusababisha ugomvi ambapo Wine alipata majeraha wakiongeza kwamba uchunguzi utafanywa ili kufafanua ukweli.
Hapo awali, chama chake cha National Unity Platform (NUP) kilidai kuwa alipigwa risasi lakini madai hayo hayakuthibitishwa.
“Rais wetu, Bobi Wine, amepigwa risasi mguuni na polisi huko Bulindo! Tutaifahamisha nchi kuhusu hali yake,” ilisomeka chapisho kwenye akaunti yake ya X.
Wine, mwanamuziki wa pop aliyegeukia siasa jina lake halisi ni Robert Kyagulanyi na alishika nafasi ya pili katika uchaguzi wa rais wa 2021 nyuma ya Museveni, ambaye ameiongoza nchi hiyo ya Afrika Mashariki kwa takriban miongo minne.