NA EUNICE KANUMBA –SHINYANGA
Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga wamepitisha mapendekezo ya mpango na bajeti ya halmashauri hiyo kwa mwaka wa fedha 2025/2026, ambapo jumla ya shilingi 40,271,905,280/= zinatarajiwa kukusanywa kutoka vyanzo mbalimbali na zitatumika katika shughuli za utoaji huduma, utawala na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Mapendekezo haya yamewasilishwa katika Mkutano Maalum wa Baraza la Madiwani uliofanyika leo, Januari 30, 2025 katika ukumbi wa kalinjuna uliopo katika manispaa hiyo ambapo madiwani hao wamekubaliana kuidhinisha bajeti hiyo na kutoa ushauri wa kuboresha baadhi ya maeneo hususan katika huduma ya maji safi na salama, na miuondo mbinu ya barabara katika baadhi ya maeneo.
Akitoa taarifa kuhusu Mapendekezo ya Mpango na Bajeti ya Halmashauri hiyo kwa mwaka wa fedha 2025/2026, Mkuu wa Divisheni ya Mipango na Uratibu wa Manispaa ya Shinyanga, Mensaria Mrema, amesema kuwa fedha zitakazokusanywa zinatokana na vyanzo mbalimbali vya mapato, ikiwa ni pamoja na Vyanzo vya mapato ya ndani Shilingi 6,403,000,000/= na Ruzuku ya miradi ya maendeleo kutoka Serikali Kuu Shilingi 6,497,592,000/=
Vyanzo vingine ni Ruzuku ya matumizi mengineyo: Shilingi 1,357,940,000/=, Ruzuku ya mishahara: Shilingi 22,219,049,200/= na Ruzuku ya miradi ya maendeleo kutoka Wahisani: Shilingi 3,794,324,080/=.
Aidha, Mrema ameeleza kuwa katika utekelezaji wa mpango wa mwaka 2024/2025, Halmashauri ilikusanya jumla ya shilingi 3,465,718,440.18/-, sawa na asilimia 54% ya makadirio ya mapato ya ndani.
“Mwaka wa fedha 2024/2025 Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga ilipanga kukusanya shilingi 38,053,453,654/= ambapo kwa kipindi cha nusu mwaka (Julai 2024 hadi Desemba 2024) imeweza kukusanya jumla ya shilingi 3,465,718,440.18/- sawa na asilimia 54% ya makadirio yote yanayotokana na vyanzo vya ndani”,amesema Mrema
Naye mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga, Mhe. Elias Ramadhani Masumbuko, amesisitiza kuwa mapendekezo hayo ni hatua ya mwanzo na madiwani bado wanaruhusiwa kutoa maoni kwa ajili ya marekebisho zaidi.
Ameshauri kuboreshwa kwa mifumo ya ukusanyaji mapato kwa kutumia busara, kuepuka kutumia nguvu na badala yake wazingatie sheria na taratibu.
Kwa upande wake Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, David Lyamongi, ameipongeza Halmashauri ya manispaa hiyo kwa maendeleo inayoyafanya katika ukusanyaji mapato na ameshauri elimu zaidi itolewe kwa wananchi kuhusu ulipaji kodi na ushuru, ili waweze kulipa kwa hiari kwa ajili ya maendeleo ya jamii
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, Revocatus Lutunda, ameahidi kutekeleza ushauri na maelekezo yaliyotolewa na viongozi katika mkutano huo.
Ajenda kuu za kikao hicho zilijumuisha kupitia mapitio ya mpango wa bajeti ya mwaka 2023/2024, nusu ya mwaka wa fedha 2024/2025, mapendekezo ya mapato ya ndani kwa mwaka 2025/2026 na mapendekezo ya mpango na bajeti kwa mwaka wa fedha 2025/2026.