Na Gideon Gregory – Dodoma.
Katika dunia inayozidi kuthamini ubunifu na ujumuishi, kuna hadithi zinazovutia ambazo zinathibitisha kuwa hakuna kikomo kwa ndoto za mtu, Moja ya hadithi hizo ni ya Bhoke Manyori, mbunifu wa mavazi mwenye ulemavu Mkazi wa Jiji la Dodoma ambaye amebadilisha mtazamo wa jamii kuhusu uwezo wa watu wenye ulemavu katika sekta ya mitindo.
Akizungumza na Jambo FM Bhoke anasema alianza kazi ya kushona mwaka 2003 baada ya kuhitimu kidato cha Nne na alipoenda kuomba kazi sehemu mbalimbali lakini hakuweza kufanikiwa ndipo akaingia kwenye sekta ya ushonaji na ubunifu wa mavazi.
“Katika hii kazi sio kwamba nilisukumwa na mtu kujifunza hapana ni mimi mwenyewe nilipenda kujifunza kwasababu nilitamani kuwa fundi na mbali ya kuwa fundi iwe moja ya ajira yangu,” anasema.

Bhoke alizaliwa na ulemavu lakini hakuacha hali yake hiyo kuwa kikwazo katika kufanikisha ndoto yake hivyo anasema anahisi alizaliwa na karama hiyo kwani alipofanikiwa kujua kushona na kubuni mitindo mbalimbali milango ya mafanikio kupitia sekta hiyo ikaanza kufunguka.
“Kwakweli nashukuru mapokezi ya familia yangu juu ya suala hilo yalikuwa mazuri na waliipenda nakumbuka wateja wangu wa kwanza nilianza na familia yangu, nilimwambia mama yangu nunueni vitambaa vya familia kwahiyo mimi nilianza kushonea familia yangu,” anaesema.

Anasema baada ya kuanza kushona familia yake walipokea na mpaka sasa mama yake anaikubari kazi yake ya ushonaji na alimpatia watumishi wenzake wakawa wateja wake na kuongeza kuwa pamoja ya kuwa huyo ni mazazi wake hakuwahi kumshonea bure naye analipa kama wateja wengine.
Juhudi za Bhoke katika sekta ya ushonaji na ubunifu wa mavazi anasema zimepokelewa kwa shangwe na jamii na hata kupelekea kupongezwa na viongozi mbalimbali wa Serikali huku akiwa ameshiriki katika maoenyesho yaliyompatia fursa ya kujitangaza kwa wengine.
“Kiongozi ambaye nilianza naye kufanya kazi ni Mkuu wa Mkoa wa Njombe Athony Mtaka kipindi yupo Dodoma, nakumbuka nilimshonea vazi la kaunda suti na hata sasa hivi nikikutana naye akiwa na watu anawaambia jamani huyu ni fundi wangu japo kuwa alihama lakini tukikutana kwenye matukio lazima aniite,” amesema.

Anaendelea kusema,”Bado kuna Mkuu wa Mkoa wetu Rosemary Senyamule nayeye pia nilimtengenezea kazi yake nzuri, niliwahi kumfanyia kazi Rais Samia nakumbuka ile tuliharikwa kwenye hafla ya watu wenye ulemavu Ikulu Chamwino, kwahiyo kuna nguo nilimtengenezea.
Bhoke anaendelea kusema japo alimtengenezea Rais nguo lakini hawezi kujua ni nani aliitengeneza na hata kama hajaivaa kikubwa aliipokea ila anaamini ipo siku ambayo haina jina atakuja kumtafuta.
Je, matamanio ya Bhoke ni yapi?
Bhoke anasema matamanio yake ni kumvalisha siku moja Spika wa Bunge na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Dkt. Tulia Ackson kabla ya kutoka kwenye uongozi wake huo.

“Usitake kutamani kumvalisha mtu mmoja, unatakiwa utamani kuvalisha hata viongozi wengi Dkt. Tulia amebeba muhimili wa Serikali kwahiyo akivaa naamini nayeye kama kiongozi mkubwa kavaa vazi kutoka kwangu, kwahiyo huyo ndiye natamani sana sana kumvalisha kwasasa,”anasema Bhoke.
Bhoke anawatia moyo watu wenye ulemavu kwamba wasisite kufuata ndoto zao kwani sio mwisho wa kujituma na kuamini katika uwezo wao, hivyo wanaweza kufanikisha chochote wanachotaka katika maisha yao.
“Kuzaliwa mlemavu sio mkosi kama ilivyokuwa inachukuliwa zamani lakini mimi nimekuja kuona kuzaliwa na mlemavu ni kusudio la Mungu kwani aliweka mtu mwenye ulemavu ili watu wote tuheshimiane kwamba inawezekana wewe ukawa mzima lakini ukashindwa kufanya kitu ukawa ni mlemavu wa akili lakini akawa huyu mlemavu wa viungo, asiyeona akafanya kitu kikubwa kuliko hata huyo asiye na ulemavu,” anasema.

Anaongeza kuwa anataka sasa kumtia moyo mwenye ulemavu kuwa na kumjenga kiimani kwamba asikate tamaa kwasababu Mungu anapokuwa amemuumba mwenye ulemavu anakusidio lake.
Hadithi ya Bhoke ni ushuhuda tosha kuwa ubunifu haujui mipaka kwamba kila mtu anayo nafasi ya kung’ara katika kile anachokipenda, kwa juhudi zake anaweza kubadilisha tasnia ya mitindo na kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa ujumuishi katika kila sekta.