Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), imetangaza bei mpya za kikomo za bidhaa za mafuta ya petroli nchini ambapo kwa Mkoa wa Dar es Salaam Petrol imepanda kwa Sh 295 kwa lita na kufikia Sh 4,115 mwezi Mei 2026 kutoka Sh 3,820 ya mwezi uliopita.
Taarifa ya EWURA imeeleza kuwa, bei hizo mpya za kikomo za mafuta zitakazoanza kutumika kuanzia Mei 6, 2026 saa 6:01 usiku, dizeli itauzwa kwa Sh 4,248 kwa lita huku mafuta ya taa yakifikia Sh 4,677 kwa lita katika jiji la Dar es Salaam.

Ongezeko hilo, limechangiwa na kupanda kwa bei za mafuta katika soko la dunia kutokana na kuendelea kwa mvutano wa kisiasa na vita katika eneo la Mashariki ya Kati, hususan kati ya Marekani, Israel na Iran.
Kufuatia tangazo hilo, EWURA imewataka Wafanyabiashara kuuza mafuta kwa bei elekezi na si vingine, huku Wnanchi wakitakiwa kuripoti vituo vitakavyokiuka agizo hilo.