Serikali imesema kuna viashiria vya kupanda kwa bei za mafuta katika bei zitakazotangazwa mwezi Oktoba, 2023 sababu zikiwa ni zilezile zilizoelezwa mwezi uliopita.
Kwa mwezi Septemba bei ya Petroli iliongezeka kwa Sh14 kwa lita moja huku dizeli ikiongezeka kwa Sh324 jambo lilioibua minong’ono miongoni mwa wananchi hususani watumiaji wa vyombo vya moto huku wachumi wakitahadharisha ongezeko la gharama za maisha.
Uwezekano huo ulidokezwa leo Jumamosi Septemba 30, 2023 na Msemaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Titus Kaguo ambaye amesema hakuna namna ya kukwepa ongezeko la bei mafuta kwani hata katika soko la dunia hali bado si nzuri.
Kaguo ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu EWURA kuvifungia vituo vya mafuta ambavyo vilionekana kukiuka sheria za manunuzi hata walipoelekezwa lakini walishindwa kufanya inavyotakiwa.