KATIBU BAVICHA AMPINGA MWENYEKITI BAVICHA SHINYANGA….

Wajumbe wa Baraza la Vijana wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA  (BAVICHA) mkoa wa Shinyanga wamepinga kauli iliyotolewa na Mwenyekiti wa Baraza hilo mkoani humo Samson Vuga kuwa wanamuunga mkono mgombea wa nafasi ya Uenyekiti wa Baraza hilo Taifa Wakili Deogratius Mahinyila.

Kauli hiyo imetolewa kwa niaba ya wajumbe hao na Katibu wa BAVICHA mkoa wa Shinyanga Mchungaji Emanuel Fungameza na kwamba kwa sasa wanawaunga mkono watia nia wote mpaka pale Chama kitakapokamilisha taratibu za usaili na kuwapata wagombea watakaowania nafasi hiyo.

“Sisi wajumbe wa mkoa wa Shinyanga Tunawaunga mkono watia nia wote,Hakuna kikao tulichomtuma Mwenyekiti kuwa tunamuunga Mkono mtia nia Deogratius Mahinyila aliyemtaja yeye,Hayo ni matwaka yake yeye na mtia nia wake” Amesema Fungameza.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza hilo Wilaya ya Shinyanga anayeongoza majimbo ya Solwa na Shinyanga mjini Alfredy Masanja amewashauri watia nia kuwasiliana moja kwa moja na wajumbe ili kuondoa mkanganyiko huku Mwenyekiti wa BAVICHA Wilaya ya Kahama Maarifa Chagula akisema hatua aliyoichukua Mwenyekiti wao wa mkoa inamchonganisha mtia nia huyo na wajumbe.

“Nitoe rai kwa watia nia kama unahitaji kuomba kura wawapigie simu wajumbe wao ndo wanajua wamchague nani,sisi wajumbe hatuna mtu wetu mfukoni hadi usaili wa chama utakapokamila,Amesema Masanja,”Hatua aliyofanya Mwenyekiti wetu wa mkoa ni kuwachonganisha wajumbe na mtia nia” Ameongeza Chagula. 

Tarehe 06 january 2025 kupitia vyombo vya habari Jijini Dodoma Mwenyekiti wa BAVICHA Mkoa wa Shinyanga Samson Vuga alinukuliwa akisema kuwa kwa kauli moja vijana wa Chama hicho mkoani humo wanamuunga mkono Wakili Deogratius Mahinyila kuwa mwenyekiti wa Bavicha Taifa.

“Mkoa wa Shinyanga tumefanya tathimini kwa muda na tumebaini kwamba wakili Deogratius Mahinyila ni kiongozi imara  anayetosha kuwa Mwenyekiti wetu wa baraza la vijana ngazi ya Taifa,Wote mnafahamu namna ambavyo wakili Mahinyila amekuwa mstari wa mbele katika mapambano ya kudai haki katika taifa letu” Amenukiliwa Mwenyekiti Vuga katika taarifa yake kwa vyombo vya Habari Dodoma.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *