
BARAZA la Sanaa la Taifa (BASATA) na MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) kwa Pamoja wameingia makubaliano ya kubadilishana taarifa na kusomana katika mifumo ya kudhibiti mapato yatokanayo na wasanii, ikiwamo kubaini wasanii wanaolipa na wasiolipa kodi nchini.
Kamishna Mwenda alisema hiyo ni katika utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan kutaka taasisi za umma, makampuni kusomana kwa taarifa.
Mwenda alisema mifumo hiyo itaweza kubaini na kutambua ni wasanii gani na wangapi wamesajiliwa TRA na kujua ambao hawajasajiliwa ili waweze kuwasaidia kutambulika kuwasajili na kupata TIN namba kwa gharama kidogo.
Mwenda alifafanua kwa kusema msaniii atakayekuwa na mapato ya chini ya Sh. 170,000 serikali itamsamehe, atakayekuwa na mapato yatakayozidi hapo atachangia kiasi kidogo na msanii atakayeanzisha kampuni yake akiwa na mapato chini ya Sh. milioni nne kwa mwezi, atasamehewa kulipa kodi lakini akiwa na mapato kwa mwaka kuanzia Sh. milioni saba, atachangia laki moja kwa mwezi na yule atakayekuwa na mapato ya Sh. milioni saba hadi Sh. milioni 11 atalipa kwa mwezi Sh. 250,000.
Pia akiwa na mapato kuanzia Sh. milioni 11 hadi 100 kwa mwezi, atachangia asilimia 3.5 ya kile anachoingiza.
Katibu Mtendaji BASATA, Dkt. Kedmon Mapana amesema mifumo hiyo itaeta mapinduzi na mabadiliko makubwa katika sekta ya sanaa, kwa wasanii wote wakiwamo waimbaji, wachoraji, MC, wachongaji na wengine wote wanaoingia kwenye kundi hilo.
Dkt. Mapana amesema watakwenda kuipa serikali mwamko ya kuisaidia sekta hii kwa kuwa wasanii wanalipa kodi, na kuongeza kuwa mifumo itaenda kusaidia wasaniii na wadau wa sanaa kufanya shughuli zao bila bugudha.