Na Saada Almasi, Bariadi – Simiyu.
Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Mjini Bariadi Mkoani Simiyu (BARUWASA), imetakiwa kujikita zaidi katika kutoa elimu juu ya utoaji wa ankara za maji kwa wananchi, ili kuondoa malalamiko ya kulimbikiziwa bili pamoja na ubadhilifu unaoweza kutokea kwa wasoma mita waomkadiria matumizi ya mtumiaji.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Baraza la Ushauri wa Watumiaji wa Huduma za Maji na Nishati (EWURA CCC), Hassan Minga katika ziara ya kukagua maendeleo ya mradi wa mabadiliko ya tabia nchi wa Maji ya Ziwa Victoria, unaotekelezwa kwa zaidi ya shilingi bilioni 400 mjini Bariadi na ambao unatajwa kuwa suluhisho la changamoto ya ukosefu wa hitaji hilo muhimu.

Amesema, dhumuni la Serikali ni kufikisha huduma za Maji kwa kila Mwananchi, hivyo wajibu wa mamlaka hiyo ni kutoa huduma kwa mujibu wa kanuni zilizopo na kuhakikisha wanatatua malalamiko yaliyopo kwa wananchi juu ya Ankara wanazoletewa kila mwezi.
“Kuna matatizo makubwa katika usomaji wa mita na utoaji wa Ankara huenda wananchi hawana elimu juu ya usomaji ama baadhi ya watumishi wasio waaminifu hawawajibiki ipasavyo katika kuwafanya wananchi wapate Ankara zinavotakiwa,ninashauri tutoke katika usomaji wa Ankara wa kuzunguka na tuhamie katika mita za luku hii itaongeza mapato na kumlinda mtumiaji,” amesema Minga.

Awali, Jambo Fm katika mahojiano na baadhi ya wakazi wa mkoa huo walisema kandoaaaa na changamoto za usomaji wa mita, huduma hiyo imekuwa ikipatikana kwa kusuasua huku baadhi ya maeneo wakimaliza muda wa wiki mbili bila hiduma, hali ambayo inawatesa.
“Maji yamekuwa changamoto hapa nyumbani yanaweza kukaa wiki moja ama zaidi bila kutoka na mwisho wa mwezi bili inatoka kama huduma ilikuwepo hii imekuwa changamoto kubwa kwa sababu bila maji hakuna kinachofanyika,” alisema Happiness Mkome, mkazi wa Somanda.

Akikazia hoja hiyo, Mkazi wa Malambo Sabato John amesema, “haya maji ambayo tunayatumia ni maji ya visima virefu shida mojawapo yanapatikana kwa uchache na bado yanachumvi nyingi kiasi kwamba tunalazimika kuweka gharama zingine kununua maji ya kunywa ya viwandani ni matumaini yangu mradi huu ukikamilika utapunguza gharama tulizokuwa tunatumia.”
Akijibu kuhusu changamoto hizo, Meneja wa BARUWASA, Nandi Mathias amesema hali ya upungufu wa maji inasababishwa na uchache wa vyanzo vya maji vilivyopo, ambavyo vinauwezo wa kuhudumia asilimia 48 ya wananchi, hivyo mradi huo wa Maji ya Ziwa Victoria utakuwa suluhisho.

“Hadi sasa tuna uwezo wa kuhudumia asilimia 48 ya wananchi kwakutumia visima 43 tulivyonavyo japokuwa wastani wa matumizi ni lita milioni 7 kwa siku kwa hiyo hii ni changamoto kubwa ambayo inakwenda kuisha mwezi Novemba baada ya ukamilifu wa mradi huu mkubwa wa maji kutoka ziwa Viktoria hivyo wananchi watapata afueni kwa kiasi kikubwa,” alisema Mha. Nandi.