Na Saada Almasi, Bariadi – Simiyu.
Katika kuendelea kuonyesha nguvu ya wananchi na kuthibitisha umoja na uwajibikaji kwa jamii, wakazi wa kijiji cha Kilabela kilichopo Kata ya Banemhi wilayani Bariadi mkoani Simiyu, wa vitongoji vitatu vya Buluguta, Mlimani na Duguda wameridhia kuchangishana na kujenga Shule ya awali na Msingi shikizi, ya Buluguta, ili kuwapunguzia mwendo watoto wao wanaofuata elimu katika shule ya msingi Kilabela.
Awali, watoto kutoka kijiji hicho walitakiwa kutembea umbali wa kilometa zaidi ya 6 kufuata elimu, wakikutana na vizingiti njiani ikiwemo mito ambayo kipindi cha masika hujaa maji na wakati mwingine wanyama wakali, ambao huleta madhara ikiwemo vifo.
Wakizungumza na Jambo Fm, wakazi hao wanasema, michango ambayo wamekuwa wakiichanga kwa awamu ndiyo imefanikisha ujenzi wa shule hiyo huku wakijivunia ushirikiano ambao wamekuwa nao hadi sasa.

“Tulianza kutoa shilingi elfu 15 kila kaya,baadae tukaongeza ikawa elfu 25 tukafika hadoi 30 awamu zote hizo pesa zilikuwa zinanunua mahitaji ya ujenzi wa hapa,ukweli tumekuwa na ushirikiano mzuri na hatuwezi kuishia hapa tutaendelea kuchanga ili hizi changamoto kwa watoto wetu ziishe kabisa,“ alisema Loyce Miso mkazi wa kitongoji cha Buluguta.
“Baada ya kupata changamoto kubwa ya watoto kuliwa na viboko wa mto ambao hujaa kipindi cha masika tukaona bora tufanye hili ili tusiendelee kuwapoteza zaidi ni watoto watogo maji ni mengi ya ule mto bado mwendo wa kilometa 6 kwa mtoto ni adhabu kubwa kwake afike Kilabela”Masunga Maduhu mkazi wa kijiji cha Kilabela.
Akitoa taarifa ya ujenzi huo, Afisa mtendaji wa kijiji cha Kilabela, Joyce Kubebeka amesema kuwa hadi sasa vyumba viwili na ofisi tayari vimejengwa ambavyo vinakwenda kutumika kufundishia watoto hao na baadae wataendelea na michango, ili kuongeza vyumba zaidi.
“Tayari vyumba viwili na ofisi vyenye thamani ya shilingi milioni 12 na elfu 29 kutoka katika michango ya wananchi vimejengwa na hii inaonyesha jinsi gani wananchi wa kiiji hiki wana mapenzi na watoto wao ambao wamekuwa wakiteseka kwa muda mrefu na baada hapa kuna mpango wa kuendelea na michango ili tupate madarasa zaidi ya kuwasaidia watoto wengi,” alisema.
Hata hivyo, Mtendaji huyo ameendelea kutoa wito kwa wakazi hao kuendela na ushirikiano mzuri waliojijengea kusaidiana katika hali ngumu na za faraja ili kuweka jamii salama zaidi.
Ujenzi wa shule hiyo shikizi kwa wakazi wa Kijiji cha Kilabela, ni muendelezo wa wakazi wa vijiji mbalimbali ndani ya wilaya ya Bariadi, ambao wamekuwa wakisaidia watoto wao kujenga shule shikizi na hata baadhi ya Zahanati,vili kupunguza mwendo mrefu wa kufuata huduma muhimu.


