Kufuatia ongezeko la wizi na utelekezaji wa watoto wachanga Baraza la Wazee Wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga limeiomba serikali kutoa adhabu kali kwa wale wote watakaobainika kufanya vitendo hivyo.
Wito huo umetolewa na Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Wilaya ya Kahama Gaudensia Ngaiwa wakati akizungumza na Jambo FM ambapo amesema kwa sasa wizi wa watoto na baadhi ya wanawake kutelekeza watoto ikiwemo utoaji wa mimba umeongezeka nchini.
Katika hatua nyingine baraza hilo limewataka watoto kuwalea wazazi na walezi wao ipasavyo kwa kuwapa mahitaji yote muhimu ikiwemo mavazi, chakula na matibabu na kuachana na tabia ya kuwatelekeza vituoni hususani kwa wazee wengi walio vijijini ilihali wana uwezo wa kuwalea na kuwahudumia.
Kwa upande wake katibu wa baraza la wazee taifa Anderson Lyimo ameiomba serikali kutoa bima ya afya bure kwa wazee ambao hawana uwezo wa kumudu gharama za matibabu kwakuwa wazee wengi wamekuwa wakikabiliwa na magonjwa kadha wa kadha kutokana na umri wao.