Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeidhinisha kwa wingi azimio lake la kwanza la kuunga mkono mpango wa kusitisha vita vya miezi minane kati ya Israel na Hamas katika Ukanda wa Gaza.
Azimio hilo lililoandaliwa na Marekani, limeidhinisha pendekezo la kusitisha mapigano lililotangazwa na Rais Joe Biden, ambalo Washington inasema kuwa Israel imekubaliana nalo na linatoa wito kwa kukubaliana na awamu tatu za mpango huo. Azimio hilo ambalo lilipitishwa na wajumbe 14 kati ya 15 wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kasoro Urusi tu ambayo ilijizuia, linazitaka Israel na Hamas kutekeleza kikamilifu vipengele vyake bila ya kuchelewa na bila masharti.
Suala la iwapo Israel na Hamas zitakubaliana juu ya mpango huo bado ni kitendawili, lakini uungwaji mkono mkubwa wa azimio hilo katika chombo chenye nguvu zaidi cha Umoja wa Mataifa, kunazidisha shinikizo zaidi kwa pande zote mbili kuidhinisha pendekezo hilo.
Afisa mwandamizi wa Hamas Sami Abu Zuhri Kundi la Hamas amesema kundi hilo linakubaliana na azimio hilo na liko tayari kwa majadiliano juu ya vipengele vilivyomo, akiongeza kuwa ni wajibu wa Washington kuhakikisha kwamba Israel inaheshimu mpango huo na miongoni mwa aliyoyataja afisa huyo kuhusu mpango huo ni kuondolewa kwa vikosi vya Israel na kubadilishana wafungwa wanaoshikiliwa na Israel.
Blinken amekutana na rais wa Israel Isaac Herzog kama sehemu ya juhudi zinazoendelea za upatanishi zinazofanywa na Marekani, Qatar na Misri za usitishaji mapigano kupitia ziara ambayo inanuia kupata uungwaji mkono wa azimio la hivi karibuni ambalo litatekelezwa kwa awamu tatu.
Mwandiplomasia huyo anatarajiwa kuhudhuria mkutano wa kiutu kwa ajili ya Ukanda wa Gaza, ambao unafanyika Jordan siku ya Jumanne ya leo Juni 11,2024, Mkutano uliopewa jina la “Wito wa hatua,hatua za haraka za kibinadamu kwa Gaza, umeandaliwa na Jordan, Misri na Umoja wa Mataifa ukitarajiwa kuhudhuriwa na viongozi, mawaziri wa mambo ya kigeni na maafisa kutoka nchi 75 pamoja na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa ikiwemo shirika la kimataifa la msalaba mwekundu.