Bado Unakatiwa Nyama Kwenye Gogo Buchani?

Na Gideon Gregory,Dodoma

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Alexender Mnyeti amesema matumizi ya magogo kwenye bucha hususani maeneo ya mjini umepungua jambo linalonesha wadau wameendelea kutekeleza katazo la Bodi ya Nyama la matumizi hayo.

Naibu Waziri Mnyeti ameyabainisha hayo leo Mei 22,2024 Bungeni Jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mhe. Toufiq Turky Mbunge wa Mpendae aliyetaka kujua ni lini katazo la Bodi ya Nyama Tanzania la kuzuia matumizi ya magogo kukatia nyama litafanyiwa kazi ili kuwanusuru watanzania kupata athari za kiafya.

Amesema Mwaka 2018, Bodi ya Nyama ilitoa tangazo kwa Umma kuhusu katazo la matumizi ya magogo katika maduka ya nyama (Bucha). Kufuatia katazo hilo, Mamlaka za Serikali za Mitaa zilijulishwa na kuhimizwa kusimamia utekelezaji wake.

“Katika kuhakikisha katazo hilo linaendelea kutekelezwa, Bodi ya Nyama imeendelea kufanya kaguzi za mara kwa mara kwenye bucha kutoa leseni za bucha kwa wafanyabiashara waliokidhi vigezo ikiwa ni pamoja na kuwa na mashine ya kukatia nyama na kutoa mafunzo kwa wamiliki na wafanyakazi kwenye bucha kuhusu uendeshaji wa maduka ya nyama, matumizi ya sahihi ya vifaa vya buchani, uhifadhi wa nyama na madhara ya matumizi ya magogo katika kukatia nyama”,amesema

Ameongeza kuwa Bodi ya Nyama kwa kushirikiana na Mamlaka za Serikali za Mitaa itaendelea kutoa elimu kwa Umma kuhusu katazo la matumizi ya magogo na kusimamia utekelezaji wake ili kuzalisha nyama bora na kulinda afya ya walaji.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *