Serikali imeelekeza watumishi wa umma katika Mkoa wa Dar es Salaam wafanyie kazi nyumbani isipokuwa watumishi ambao mazingira ya kazi yanawataka kuwepo katika vituo vya kazi, kutokana na Tanzania kuwa mwenyeji wa Mkutano Mkuu wa Nchi za Afrika wa Nishati utakaofanyika Januari 27-28, 2025 nchini.
Watumishi hao ni wa vyombo vya ulinzi na usalama, sekta ya afya na sekta ya usafiri na usafirishaji, ambapo Benki, Hoteli na Migahawa hazitafungwa na biashara katika soko la Kariakoo ambazo zitaendelea kufanyika.
Taarifa hiyo iliyotolewa na Ofisi ya Rais Ikulu kupitia Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dkt. Moses Kusiluka imesema waajiri katika Sekta binafsi wanashauriwa kuruhusu watumishi wao katika Mkoa wa Dar es Salaam kufanyia kazi zao nyumbani au kuweka utaratibu ambao hautasababisha changamoto ya usafiri kutokana na kufungwa kwa baadhi ya barabara muhimu.