Uamuzi wa jopo la Majaji wa New York kumtia hatiani Rais wa zamani unaonyesha hakuna mtu aliye juu ya sheria, inasema kampeni ya Biden
Hukumu ya kihistoria ya rais wa zamani wa Marekani Donald Trump katika mahakama ya New York nchini Marekani kwa makosa 34 ya uhalifu siku ya Alhamisi iliibua hisia kali kutoka kwa pande zote za kisiasa.
Kampeni ya mpinzani wa Trump katika uchaguzi, na mgombea urais wa chama cha Democratic, Rais Joe Biden, imesema uamuzi wa jopo la majaji wa New York kumtia hatiani rais wa zamani unaonyesha kuwa hakuna mtu aliye juu ya sheria.
Kwa upande wa timu ya Trump ilidai kwamba Donald Trump hakuweza kutendewa haki kwenye kesi katika moja ya maeneo yenye uhuru zaidi katika taifa na wakati huo huo, Spika wa Baraza la Wawakilishi Mike Johnson, ambaye ni kiongozi wa ngazi ya juu wa Republican baada ya hukumu hiyo alisema Leo (Alhamisi ya Mei 30) ni siku ya aibu katika historia ya Marekani.
Kura za maoni zinaonyesha kuwa kupatikana na hatia kwa Trump huenda kukamsababishia hatari katika uchaguzi ambao unaweza kuamuliwa tu kwa kura katika majimbo machache.
Katiba ya Marekani inaweka masharti machache ya kustahiki kwa wagombeaji urais: lazima wawe na angalau miaka 35, wawe raia wa Marekani “wazaliwa asili na wameishi Marekani kwa angalau miaka 14 na hakuna sheria zinazozuia wagombea walio na rekodi za uhalifu.
Lakini uamuzi huu wa hatia bado unaweza kuathiri uchaguzi wa urais wa Novemba. Kura ya maoni kutoka kwa Bloomberg na Morning Consult mapema mwaka huu iligundua kuwa 53% ya wapiga kura katika majimbo muhimu yanayoweza kuamua mshindi wa uchaguzi wangekataa kumpigia kura mgombea wa Republican ikiwa atapatikana na hatia.
Kura nyingine ya maoni, kutoka Chuo Kikuu cha Quinnipiac mwezi huu, ilionyesha 6% ya wapiga kura wa Trump wangekuwa na uwezekano mdogo wa kumpigia kura hatua ambayo itaathiri matokeo katika kinyang’anyiro kikali kama hicho.