Na Eunice Kanumba – Shinyanga.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga kupitia kitengo cha maendeleo ya jamii imeanza rasmi maandalizi ya uzinduzi wa kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia Legal Aid, unaotarajiwa kufanyika Mei 5, 2026 katika viwanja vya Zimamoto, Manispaa ya Shinyanga.
Akizungumza katika kikao kazi, cha uzinduzi wa kampeni hiyo, Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka ofisi hiyo, Rehema Edson, amesema kuwa mkoa huo umepata fursa ya kuwa miongoni mwa maeneo yatakayofaidika na awamu ya pili ya kampeni hiyo.

Ameeleza kuwa kampeni hiyo itazinduliwa mei 5, 2026 ikiwa na lengo la kuwafikia wananchi wengi zaidi, hususan wale wasio na uwezo wa kumudu gharama za huduma za kisheria.
Akizungumzia awamu ya kwanza ya kampeni hiyo Rehema amesema kuwa katika awamu ya kwanza, idadi kubwa ya wananchi wa Shinyanga walionyesha uhitaji mkubwa wa msaada wa kisheria, hali iliyochochea serikali kuanzisha awamu ya pili ili kupanua huduma hizo na kupunguza changamoto za kisheria katika jamii.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Sheria katika ofisi hiyo, wakili Dinah Kihanga, amesema kampeni hiyo inalenga kuwafikia wananchi wa halmashauri zote sita za mkoa wa Shinyanga na inatarajiwa kudumu kwa siku 15.
Kampeni ya msaada wa kisheria inayojulikana kama Mama Samia Legal Aid Campaign imeendelea kutoa huduma muhimu kwa wananchi nchini Tanzania, hususan makundi yenye uhitaji mkubwa wa msaada wa kisheria. Mpango huu ulioanzishwa chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan ukilenga kuongeza upatikanaji wa haki kwa kutoa elimu ya sheria, ushauri wa bure, na uwakilishi kwa wananchi wasio na uwezo.

Kupitia kampeni hiyo, maelfu ya wananchi tayari wamefikiwa katika mikoa mbalimbali, wakipata ufumbuzi wa migogoro ya ardhi, masuala ya familia, na haki za binadamu, Serikali imeeleza kuwa itaendelea kuimarisha kampeni hii ili kuhakikisha haki inapatikana kwa wote bila vikwazo na sasa ikitarajiwa kuingia katika awamu ya pili.


