ATHARI ZA MVUA ITILIMA: KAYA 16 ZAKOSA MAKAZI

Na Saada Almasi, Itilima – Simiyu.

Zaidi ya familia 112 zilizopo Wilayani Itilima mkoani Simiyu, zimeathirika kutokana na mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali kunyesha usiku wa kuamkia Aprili 8 2025 na kubomoa nyumba 34 huku kaya 16 zikiachwa bila makazi.

Jambo Fm imefika katika maeneo hayo na kuzungumza na mwenyekiti wa kitongoji cha Sokoine kijiji cha Inalo wilayani humo Limbu Deus ambaye amesema kuwa mvua hiyo iliyoanza majira ya saa nne za usiku na kukatika saa tisa usiku imeleta athari kubwa katika nyumba ambazo zilijengwa kwa kutumia matofali ya matope ambayo yalikuwa rahisi kurojeka wakati wa mvua hiyo.

“shida huku watu wanajenga nyumba kwa kutumia matofali ambayo si imara ni ya tope yakikutana na mvua yanakunywa maji kirahisi na kuanza kubomoka ukiwaambia kutumia matofali ya saruji wanasema hali ya kiuchumi ni ngumu hatumudu hayo matofali,” Mwenyekiti Limbu.

Benjamin Wilson ni mmoja wa waathirika ambaye wapwa wake wawili walinusurika kifo baada ya ukuta wa chumba walichokuwa wamelala kuangukia kitanda walichokuwa wamelala.

“ilikuwa usiku sasa mama yao alisikia kishindo kikubwa kutokea chumba cha Watoto wake alipofika alikuta tayari Watoto wameamka na kusimama pembeni ya kitanda ambacho kilikuwa kimeangukiwa na ule ukuta ndipo akawatoa lakini hadi sasa hatujui tutalala wapi”

Angalizo juu ya mabadiliko ya tabia nchi yatakayo sababisha kuwepo kwa vipindi vya mvua kubwa lilitolewa na mamlaka husika lakini bado wananchi wa maeneo mengi wilayani humo wanaishi maeneo hatarishi hasa yanayopitiwa na mikondo ya maji.

Mkuu wa wilaya hiyo Anna Gidarya amefika katika maeneo hayo kutoa mkono wa pole na kujionea hali halisi huku akiwataka wakazi wa maeneo hayo kuhama kuhama mara moja kwani kuendelea kuishi maeneo hayo kunaleta athari kwa taifa

“viongozi wa vitongoji mitaa na diwani hakikisheni hawa walioathirika wanafika mahali tulipowatengea kujistiri hadi pale tutakapopata suluhisho ambazo ni maeneo ya ghala la Isakang’wale na ofisi ya kijiji  lakini tambueni kwamba kufa kwenu ni hasara kwa serikali hivyo hameni hapa mara moja kwani uwepo wenu utaleta maafa zaidi,” alisema Mkuu wa Wilaya Anna.

Sambamba na hilo Gidarya amesema kuwa kwa sasa serikali itaendelea kufanya tathimini ya hasara iliyotokea ili kuwasaidia kuendelea na majukumu yao huku akitoa angalizo kwa wazazi kuwa makini na Watoto wao kwani kwa sasa baada ya yoo kubomolewa vinyesi vimeanza kuelea juu ya maji ambayo Watoto wanachezea

“Wakati huu serikali inaendelea na tathimini za hasara mlizopata walindeni Watoto wenu magonjwa ya mlipuko yatarudai tena kuna vinyesi vinaelea juu ya maji na maji hayo wanachezea Watoto bila tahadhari hali itakuwa mbaya,” ameongeza Gidarya.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *