Askofu wa Kanisa la Kilutheri Afrika Mashariki KKAM Nyanda za Juu Kusini, Dk Edward Mwaikali amewataka Watanzania kuliombea Taifa liendelee kuwa salama kutokana na tukio kubwa la uchaguzi mkuu linalotarajiwa kufanyika mwaka huu.
Aidha amewaomba Wakristo, wakiwamo waumini wa Usharika wa Ruanda, jijini Mbeya kujitokeza kwa wingi kuchukua fomu kugombea urais, ubunge na udiwani kupitia vyama mbalimbali vya siasa nchini ili wapate fursa ya kuwatumikia Watanzania.
Askofu Mwaikali ametoa wito huo leo Aprili 20, 2025 wakati wa ibada ya Sikukuu ya Pasaka katika Usharika wa Ruanda na kusema amani ndiyo msingi wa maendeleo ya mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
Amesema ukiwa mwaka wa uchaguzi mkuu, kila mmoja anapaswa kuwa mbele kutetea amani kama ilivyo kwa mzazi, hasa mama kwani yakitokea machafuko Tanzania, hakuna Taifa mbadala.