Matumaini ya kuendelea na masomo yamerejea kwa mtoto mwenye ualbino, Ian John, anayesoma Shule ya Msingi Mitindo Maalumu Wilayani Misungwi, baada ya Askari wa Jeshi la Polisi kutoka kundi la GH, kumkabidhi vifaa vya shule vyenye thamani ya zaidi ya shilingi laki tano.
Msaada huo uliotolewa Septemba 1, 2026, umejumuisha tranka, begi, madaftari, kalamu, nguo za shule, viatu na vifaa vingine, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 15 ya utumishi wa askari hao, walioamua kuelekeza furaha yao katika kuwasaidia watoto wenye mahitaji maalumu.

Kutolewa kwa msaada huo kunatokana na tukio la mwaka 2024, ambapo Ian akiwa na miaka miwili na miezi saba wilayani Sengerema alinusurika kutekwa kutokana na imani potofu dhidi ya watu wenye ualbino.
Wazazi wake waliripoti tukio hilo kupitia elimu ya Polisi Kata, na Polisi wakamhamishia shule hiyo kwa usalama.





