Na Tryphone Odace – Kigoma.
Jeshi la Magereza Mkoani Kigoma limejitolea kufanya usafi wa mazingira na kuchangia damu kwa ajili ya wahitaji wa damu katika Hospitali ya Manispaa ya Kigoma Ujiji ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 65 tangu kuanzishwa kwa Jeshi hilo.
Akizungumza na Jambo Media akiwa Hospitalini hapo, Mkuu wa Magereza Mkoa wa Kigoma Kamishna Msaidizi wa Magereza Musa Mkisi alisema lengo la kufika hospitalini hapo ni kudumisha na kuimarisha ushirikiano pamoja na mahusiano mazuri yaliyopo kati ya jeshi la Magereza na wananchi wanaopatiwa huduma katika hospitali hiyo kwa kujitolea kutoa damu na kutoa zawadi kwa wagonjwa.

Alisema wameamua kuwatembelea wagonjwa hospitalini hapo na kuwapatia zawadi hizo kwani sio kila mgonjwa ana uwezo wa kumudu mahitaji yote akiwa hospitali
“Ukitembelea hospitali nyingi utakutana na wagonjwa wapo ambao uwezo wao ni mdogo na hawana mtu wa kuwajali lakini tulivyoshiriki hivi hata Yule ambaye alikuwa hana kitu atajiona kuwa jamii inamjali,” alisema Mkisi.

Aidha ameitaka jamii kuendelea kuwaunga mkono wafungwa waliomaliza vifungo vyao kwa kuwa wamepata ujuzi na vyeti rasmi vinavyowawezesha kujiajiri na kujikwamua kiuchumi kwani kuwatenga wafungwa waliomaliza vifungo vyao kunaweza kuwafanya kurudia matukio ya kihalifu na kuzima ndoto zao.
Baadhi ya Maafisa Magereza wamevitaka vyombo vingine vya usalama kuendelea kuwa karibu na jamii kwa kusaidia mahitaji mbalimbali ikiwemo uchangiaji wa damu ili kuokoa maisha ya watu wengine wenye uhitaji.

Kwa upande wake, Dkt. Emanuel Onanda kutoka Hospitali ya Manispaa ya Kigoma Ujiji, amliataka wadau wengine kuendelea kuchangia damu kwani wahitaji ni wengi ikiwemo akina mama wajawazito, watoto wachanga na wanaopata ajali za barabarani.
“Kiukweli niwashukuru sana magereza kwa kuja katika hospitali yetu kuchangia damu kwani kuna uhitaji wa damu kila siku na damu haijawahi kutosha nadhani watu wengine na wadau waendelee kujitoa na kuchangia damu maana kila tunaletewa watu wanaohitaji damu hapa hospitalini” alisema Onanda.

Kuelekea miaka 65 ya kuanzishwa kwa Jeshi la Magereza, Jeshi hilo limeendelea kutekeleza shughuli mbalimbali za kijamii ikiwa ni sehemu ya kuimarisha uhusiano na jamii pamoja na kushiriki katika shughuli zenye manufaa kwa wananchi.




