ASILIMIA 20 YA WATOTO WANAOZALIWA BUGANDO HUKUMBWA NA TATIZO LA MOYO

Takribani asilimia 20 ya watoto wachanga wanaozaliwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando (BMC) jijini Mwanza hukumbwa na matatizo ya moyo, ambapo nusu yao huhitaji upasuaji ili kuokoa maisha.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali hiyo, Sista Alicia Masenga wakati akizungumza kwenye maadhimisho ya Siku ya Moyo Duniani yaliyofanyika hospitalini hapo ambapo amesema changamoto kubwa inayokwamisha matibabu ni ukosefu wa maabara maalumu ya moyo (Cath Lab), jambo linalosababisha wagonjwa wengi kuhitaji rufaa nje ya Bugando.

“Miaka minane iliyopita tuliwahi kufanya upasuaji wa moyo wa wazi kwa wagonjwa zaidi ya 100, lakini huduma hiyo imesimama kutokana na ukosefu wa vifaa muhimu kama Heater Cooler, mashine za uchunguzi na wataalamu,” amesema Masenga.

Katika hatua nyingine Alicia amesema kuwa tangu mwaka 2007, takribani wagonjwa 2,000 wakiwemo watoto na watu wazima hufaidika kila mwezi na huduma za moyo hospitalini humo, lakini wengi hushindwa kupata matibabu kwa wakati unaofaa na hivyo kufikia hatua ya kupata madhara makubwa kiafya.

Kwa upande wake Daktari bingwa wa moyo wa watoto, Julieth Kabirigi, amesema idara hiyo hupokea watoto kati ya 20 hadi 40 kila wiki, sawa na 200 hadi 240 kwa mwezi, huku asilimia 40 hadi 50 wakigundulika na matatizo ya moyo ya kuzaliwa au yanayosababishwa na maradhi mbalimbali. Alitaja visababishi vikuu kuwa ni maambukizi wakati wa ujauzito, lishe duni, changamoto za kimaumbile, urithi, na maradhi ya koo yanapochelewa kutibiwa.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dk Jesca Lebba, amesema kuwa kati ya watu 225,000 waliopata huduma za magonjwa yasiyo ya kuambukiza mwaka 2024, zaidi ya 5,000 waligundulika kuwa na matatizo ya moyo, wakiwemo waliotibiwa Bugando.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, amewataka wananchi kubadili mtindo wa maisha, kula vyakula vyenye lishe bora, kuepuka ulaji usiofaa, pombe, tumbaku na uzito mkubwa, pamoja na kufanya mazoezi mara kwa mara.

“Serikali inahimiza ukaguzi wa mara kwa mara wa afya ili kubaini mapema magonjwa na kuepuka gharama kubwa za matibabu. Changamoto ya magonjwa katika jamii yetu ipo, tusijifiche katika nyumba zetu tujitokeze tufanye vipimo mapema kujua tatizo,” amesema Mtanda.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *