
Hii leo Waafrika Kusini kupitia kura zao watakazopiga katika uchaguzi wa leo wataamua katika kura tatu tofauti kudhibiti Bunge na mabunge tisa ya majimbo.
Uchaguzi huo ndio utakaoamua iwapo chama cha African National Congress (ANC), kinachoongozwa na Rais Cyril Ramaphosa, kinaweza kudumisha mshikamano wake wa miaka thelathini kwa wapiga kura au iwapo chama kilichotawala tangu kumalizika kwa ubaguzi wa rangi kitalazimika kuunda muungano kwa mara ya kwanza.
Waafrika Kusini wanapiga kura katika uchaguzi muhimu zaidi tangu mfumo wa ubaguzi wa rangi kumalizika mwaka 1994 na zaidi ya watu milioni 27 wamejiandikisha kupiga kura katika kura inayoangazia kuongezeka kwa mgawanyiko wa kisiasa baada ya miaka 30 ya demokrasia,Vyama 70 na wagombea huru 11 wanashiriki katika uchaguzi ambao utashuhudia Waafrika Kusini wakipigia kura bunge jipya, na mabunge tisa ya majimbo.

Kikiwa madarakani tangu aliyekuwa mpinga wa ubaguzi wa rangi Nelson Mandela alipoongoza kwa ushindi mwishoni mwa utawala wa wazungu wachache, chama cha African National Congress (ANC) kinawania muhula wa saba madarakani na ingawa kina uhakika wa ushindi kura za maoni zimekuwa zikionesha mara kwa mara kuwa chama hicho kitapoteza wingi wake wa wabunge kwa mara ya kwanza, na kukilazimisha kuingia katika muungano na chama kimoja au zaidi cha upinzani.
Lakini Kampeni za kuelekea uchaguzi wa leo zilitawaliwa na ufisadi ulioenea serikalini, viwango vya juu vya ukosefu wa ajira, haswa miongoni mwa vijana, kuzorota kwa huduma za umma na uhalifu uliokithiri.

Chama kikuu cha upinzani cha Democratic Alliance (DA) kimesaini mkataba na vyama vingine 10, kukubaliana kuunda serikali ya mseto iwapo watapata kura za kutosha kukiondoa chama cha ANC mamlakani hilo linaonekana haliwezekani sana, huku ANC ikitarajiwa kubaki chama kikubwa zaidi, na kukiweka katika nafasi nzuri ya kuongoza muungano.


