Serikali inaendelea na juhudi za kutafuta mwekezaji mahiri mwenye nia thabiti ambaye atawekeza katika kiwanda cha Nyama kilichopo mkoani Shinyanga ili kiweze kufanya kazi iliyokusudiwa kwa maslahi ya Taifa.
Hayo yameelezwa leo Bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Alexander Mnyeti wakati akijibu swali la Mhe. Dkt. Christiana Mnzava Mbunge wa Viti Maalum aliyetaka kujua Serikali ina mpango mkakati gani juu ya kiwanda hicho ambacho hakifanyi kazi iliyokusudiwa.
“Kiwanda cha nyama cha Shinyanga ni miongoni mwa viwanda vitatu (3) vya nyama vilivyokuwa vinamilikiwa na Kampuni ya Tanganyika Packers Limited (TPL),”amesema.
Mnyeti ameongeza kuwa kiwanda kilianza kujengwa 1975 na kilikamilika 1978 kwa asilimia 84% lakini hakijawahi kufanya kazi na kuongeza kuwa kilibinafsishwa kwa kampuni ya Triple S Beef Ltd, mwaka, 2007.
“Hata hivyo, mwekezaji hakuweza kuendeleza kiwanda hicho kulingana na makubaliano ya mkataba wa ubinafsishaji jambo lililopelekea Serikali kuamua kukirejesha mwaka 2017 na kwa sasa kiwanda kipo chini ya usimamzi wa Ofisi ya Msajili wa Hazina,”ameongeza.