Jeshi la Polisi Mkoa wa Mtwara linamshikilia Osward Dady, mkazi wa Mtaa wa Luchingu Halmashauri ya mji Newala, anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 35-40, kwa tuhuma za kumuua kwa mkata koromeo mtoto mwenye umri wa miaka Mitatu Nazareth Mustapha.

Akitoa taarifa ya tukio hilo lililofanyika Novemba 08, 2023 katika Mtaa huo, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara Kamishna Msaidizi wa Polisi Mtaki Kurwijila, amesema mtuhumiwa alitekeleza mauaji hayo kwa kutumia kitu chenye ncha kali na kuuhifadhi mwili ndani ya mfuko wa Shangazi Kaja.
Mtaki amesema Mtoto huyu alikuwa akicheza na wenzake nyumba ya jirani na mtuhumiwa anapokaa, baada ya muda mtuhumiwa alimuita ndani mtoto akaingia ndani, lakini baada ya kuingia ndani wakati watoto wenzake wanaendelea kucheza nje alifanikiwa kumkata kwenye koromeo na kusababisha kutoka damu nyingi na hatimae kusababisha kifo cha huyo mtoto.