Polisi nchini Uganda wanamshikilia mzee wa miaka 110 kwa tuhuma za kumchoma kisu hadi kufa mkewe mwenye umri wa miaka 109 kwa kumnyima unyumba.
Msemaji wa jeshi la polisi Samson Kasasira amenukuliwa akisema kuwa usiku wa kuamkia jumamosi majira ya saa nane , marehemu alikataa ombi la mume wake la kutaka kuambatana naye kitandani kwa sababu alikuwa anaishiwa nguvu na alikuwa na kikohozi.
“Wawili hao walienda kulala katika vyumba tofauti na marehemu akihamia chumba cha wajukuu zake wawili,” msemaji wa polisi alisema. Siku iliyofuatia wajukuu walisikia vurugu na walipokwenda kupeleleza babu aliwafukuza na “Ndipo mshukiwa alianza mara moja kumchoma kisu marehemu mara kadhaa, na kumlazimu mjukuu mwingine kukimbia na kutafuta msaada kwa majirani.”
Majirani walipofika walimkuta bi Bakasisa akiwa amefariki , huku Babiiha akiwa amejifungia chumbani ambapo alikutwa amepoteza fahamu huku pembeni yake akiwa na chupa ya kemikali ya kilimo.