Aliyewaua watoto wake wawili kwa sumu naye afariki

Mama wa watoto wawili Mario Semen (4) na Beonis Semen (2), Daines Mwashambo (30), aliyewaua wanae hao kwa kuwanyweshwa sumu nae amefariki katika Kijiji cha Mashese Mkoani Mbeya.


Kamanda wa Polisi Mkoani humo Benjamin Kuzaga amethibitisha kifo hicho ambapo amesema kuwa marehemu alikuwa akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Mkoa wa Mbeya na amefariki dunia Machi 9 Saa 10:15 jioni.


Kamanda Kuzaga amesema kuwa marehemu akiwa nyumbani kwake Kijiji cha Mashese – Ilungu aliwanywesha sumu watoto hao, kisha na yeye alikunywa sumu hiyo iliyopelekea kukimbizwa Hospitali ya Mkoa wa Mbeya kwa ajili ya matibabu.


Mtuhumiwa aliendelea kupatiwa matibabu hospitalini hapo akiwa chini ya ulinzi, lakini Machi 9 akafariki dunia.


Amesema kuwa uchunguzi wa awali ulibaini kuwa tukio la mama huyo kuwaua wanae na kujaribu kujiunga na yeye imetokana na msongo wa mawazo.

Jeshi la Polisi linatoa wito kwa jamii kuwa pindi unapopatwa na tatizo suluhisho lake sio kujichukulia sheria mkononi bali ni kutafuta ushauri au kufuata sheria inavyoelekeza ili kuepuka madhara kwa muhusika na jamii inayokuzunguka.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *