ALIYEMUUWA MPENZIWE AKIMTUHUMU KUMUAMBUKIZA UKIMWI ADAKWA NA POLISI

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mara linamshikilia Samweli Emmanuel (20), mkazi wa kijiji cha Nata Wilaya ya Serengeti kwa tuhuma za mauaji ya Josephina Magani (52), mkazi wa kijiji cha Nata Wilaya ya Serengeti mkoani Mara.

Taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara imeeleza kuwa, tukio hilo lilitokea Mei 7, 2025 majira ya saa 7:00 usiku katika kitongoji cha Mambaswe kilichopo Kijiji cha Nata Wilayani Serengeti, ambapo mtuhumiwa Samweli Emmanuel maarufu kama Nzaliya alimchoma Josephina Magani kwa kutumia kitu chenye ncha kali, maeneo ya tumboni na kusababisha kumwaga damu nyingi na kupelekea kufariki dunia.

“Mtuhumiwa mara baada ya kutenda kosa hilo aliuburuza mwili wa marehemu kutoka nyumbani kwake na kuutumbukiza kwenye shimo ambalo lilikuwa linatumika kwa shughuli za uchimbaji wa madini ya dhahabu kipindi cha nyuma,” ilieleza taarifa hiyo.

Aidha, uchunguzi wa awali umebaini chanzo cha tukio hilo ni ugomvi baina ya marehemu na mtuhumiwa kwa kile kinachodaiwa kuwa mtuhumiwa alikuwa anamshutumu marehemu kumuambukiza maradhi ya ugonjwa wa ukimwi, kwani walikuwa wakiishi kama mume na mke.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mara linatoa wito kwa wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi na badala yake watoe taarifa kwa vyombo husika ili malalamiko yao yaweze kushughulikiwa kisheria.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *