AKUTWA AMEFARIKI AKIWA MTUPU KATIKA NYUMBA YA KULALA WAGENI

Mwanamke mmoja ambae hakufahamika kwa jina na ambaye anakadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 30- 32, amekutwa amefariki dunia katika nyumba ya kulala wageni huku mwili wake ukiwa mtupu.

Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa amesema tukio hilo lilitokea majira ya saa mbili asubuhi na walipokea taarifa kuwa amefariki katika nyumba ya kulala wageni iitwayo First and Last iliyopo eneo la Usagara katika wilaya ya Misungwi.

Amesema, “mara baada ya kupokea taarifa hiyo Polisi walifika katika eneo hilo na ilibainika kuwa tarehe 18.03.2025 majira ya saa moja usiku katika nyumba hiyo ya kulala wageni alifika mgeni aliyejiandikisha kwa jina Bilal William, mkazi wa Geita akitokea Chato kuelekea Nzega mgeni huyo alipewa chumba namba tatu na kuweka mizigo yake na ilipofika majira ya saa nne usiku alitoka chumbani baada ya kudai kuwa anakwenda kutafuta chakula, na alirudi usiku wa manane akiwa na mwanamke huyo.”

Inadaiwa kuwa ilipofika majira ya saa kumi na mbili asubuhi wakati wahudumu wa nyumba hiyo ya kulala wageni wakihitaji kufanya usafi walipokuta mlango wa chumba alichokua amelala mwanaume huyo ukiwa na komeo lililofungwa kwa nje hali hiyo iliwatia mashaka.

“Hivyo walifungua kufuli hilo na kuingia ndani, na walikuta mwanamke huyo amefariki huku akiwa amefungwa usoni kwa kitambaa pamoja na mikwaruzo usoni mwake huku akiwa uchi,” alisema.

Mutafungwa amesema Mwili wa marehemu umepelekwa Hospitali ya Wilaya ya Misungwi kwa ajili wa uchunguzi na utambuzi huku pia akisema jeshi hilo linaendelea kumtafuta mwanaume huyo ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi yake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *