Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Patrobas Katambi amesema kuwa kwa mwaka 2021/2022, jumla ya ajira zilizozalishwa nchini kutokana na uwekezaji wa serikali na sekta binafsi ni 1,226,925 ambapo wastani wa ajira 670,140 kutoka miradi ya serikali kuu, serikali za mitaa, mashirika na taasisi za umma pamoja wastani wa ajira 556,785 katika sekta binafsi.
Katambi ameyasema hayo Jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari wakati akitoa maelezo kuhusiana na shughuli zinazotekelezwa na zinazoendelea kutekelezwa nchini.
Aidha ameongeza kuwa watafutakazi 578 ambapo wanawake ni 239 na wanaume ni 317 ambao wameunganishwa na fursa za mafunzo ya uzoefu wa kazi kwa kugharamiwa na Serikali. Sambamba na hayo amesema Serikali imetoa bilioni 3.46 kwa ajili ya ukarabati wa vyuo vya Ufundi stadi na marekebisho kwa Watu wenye Ulemavu vilivyopo Saba Saba -Singida, Yombo -Dar es Salaam, Mtapika -Masasi na Luanzari- Tabora.
Pia Katambi amesema serikali imeendelea kuratibu ajira za wageni ambapo jumla ya maombi 8,392 ya vibali vya kazi yamepokelewa na kufanyiwa kazi huku kati ya maombi hayo, maombi 7,729 yamekubaliwa na maombi 82 yamekataliwa kutokana na kutokidhi vigezo vya kisheria.