Ajali ya Basi yaua 12 33,Wajeruhiwa Mbeya

Taarifa rasmi kutoka Jeshi la Polisi mkoani Mbeya Imeeleza kwamba Septemba 06,2024 majira ya saa 1:30 asubuhi huko katika eneo la Lwanjilo, Wilaya ya Mbeya katika barabara ya Mbeya – Chunya, Basi la abiria lenye namba za usajili T.282 CXT aina ya Yutong mali ya kampuni ya AN Classic lililokuwa likiendeshwa na Dereva Hamduni Nassoro Salum [37] Mkazi wa Tabora likitokea Mbeya kuelekea Tabora kupitia Wilaya ya Chunya liliacha njia na kwenda kugonga gema na kisha kupinduka na kusababisha vifo, majeruhi na uharibifu wa gari.

Katika ajali hiyo watu 12 wamepoteza maisha kati yao wanaume 5 akiwemo aliyekuwa Dereva wa Basi hilo Hamduni Nassoro Salum, wanawake 7 miongoni mwao watoto wadogo 2.

Aidha, katika ajali hiyo watu 33 ni majeruhi ambao kati yao 22 ni wanaume na 11 ni wanawake. Majeruhi wanaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya, Hospitali ya Wilaya ya Chunya na Kituo cha Afya Chalangwa kilichopo Wilaya ya Chunya.

Uchunguzi wa awali uliofanywa umebaini kuwa chanzo cha ajali ni uzembe wa Dereva kushindwa kulimudu Gari lake kwenye eneo lenye mteremko na kona kali.

Jeshi la Polisi linaendelea kutoa wito kwa madereva kuwa makini na kuzingatia sheria, alama na michoro ya usalama barabarani ili kuepuka ajali zinazoweza kuepukika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *