Mgombea Ubunge wa Jimbo la Solwa kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) Ahmed Ally Salum amewaomba wana CCM kuvunja makundi yaliyokuwepo wakati wa kura za maoni kisha waungane kusaka kura, ili CCM iendelee kushika dola huku akiahidi kutatua changamoto ya maji katika kata ya Lyamidati.
Ameyabainisha hayo katika uzinduzi wa Kampeni za CCM katika uliofanyika Kata ya Lyamidati iliyopo Jimbo la Solwa wakati akinadi sera na ilani ya uchaguzi ya CCM (2025-2030) kwa Wananchi.
Amesema, mchakato wa kura za maoni umeshapita na wagombea wameshapatikana kwa ngazi zote za Ubunge na Udiwani, hivyo ni vyema makundi yote yakavujwa na kuungana kusaka kura zikiwamo za Rais Samia ili CCM ipate kushinda kwa kishindo Oktoba 29.

“Hapa Lyamidati naskia kuna makundi, naombeni wana CCM wenzangu tuvunjeni makundi yote yaliyokuwapo kipindi cha kura za maoni,sababu wagombea wameshapatikana tuunganeni tusake kura CCM ishinde kwa kishindo, kuendekeza makundi ni kujiumiza na kujipa presha bure,” amesema Ahmed.
Aidha amekipongeza pia Chama chake pamoja na wana CCM wote kwa kuendelea kumwamini na kumpitisha kugombea tena Ubunge katika Jimbo hilo la Solwa, huku akianisha kuwa hawezi kuwaangusha na atawaletea maendeleo.
Pia, ameshukuru kugawanywa kwa Jimbo hilo la Solwa ambalo awali lilikiwa na Kata 26, lakini sasa kuna Kata 12 na Jimbo jipya ya Itwangi likiwa na Kata 14 ambapo kasi ya maendeleo itaongezeka zaidi akisema amebakiwa na Kata chache.

Akielezea maendeleo yaliyofanya ndani ya miaka mitano katika Jimbo la Solwa amesema sekta ya maji kati ya vijiji 68, vitano pekee ndivyo vimebaki havina maji na kwamba katika bajeti ijayo endapo wananchi wakampatia ridhaa ya kuwa Mbunge tatizo hilo anakwenda kulimaliza.
Amesema kwa upande wa sekta ya Afya amejenga Zahanati nyingi na Vituo vya Afya, na kwamba katika Bajeti ijayo Kata ya Lyamidati itapewa kipaumbele kujengewa kituo cha Afya.
Kuhusu umeme, amesema vijiji vyote vya Solwa vina huduma hiyo isipokuwa Vitongoji vichache na pia ameboresha miundombinu ya barabara ikiwamo ujenzi wa madaraja na makaravati.

Aidha, Ahmed ameahidi wananchi kwamba akimpatia ridhaa tena, ataendelea kuwaletea maendeleo pamoja na kushughulia tatizo la Mgogoro wa Hifadhi na kuwaahidi vijana kuwa ataanzisha mashindano ya michezo, ili kuibua vipaji.
“Nawaombeni sana wananchi siku ya Uchaguzi Oktoba 29 mpigieni kura za ndiyo Rais wetu Dkt.Samia Suluhu Hassan, Mimi mwenyewe na Mgombea Ubunge wa Itwangi Dada yangu Azza Hillal Hamad na Madiwani wote wa CCM, ili tuendelee kuwaletea maendeleo,” amesema Ahmed.
Naye Mgombea Ubunge wa Jimbo la Itwangi Azza Hillal Hamad amewaomba Wananchi kwamba Oktoba 29 wasifanye makosa bali wamchague Rais Samia, Ahmed yeye mwenyewe na madiwani wote wa CCM, ili wafanye kazi kama timu na kuwaletea maendeleo.

Awali, Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Shinyanga Vijijini, Edward Ngelela amewasisitiza wananchi kwamba siku ya uchaguzi Oktoba 29 wajitokeze kwa wingi kupiga kura na kuchagua mafiga matatu ya CCM kwa kura za ndiyo kwa Rais Samia, Wabunge na Madiwani.