AFISA ELIMU SIMIYU AWATAKA WAZAZI KUCHANGIA CHAKULA CHA WATOTO MASHULENI…

NA. SAADA ALMASI -SIMIYU

Wananchi mkoani Simiyu hususan wazazi ambao Watoto wao wamejiunga na masomo katika shule mbalimbali mkoani humo wametakiwa kuweka kipaumbele katika kuchangia chakula shuleni ili mtoto aweze kupata mlo akiwa masomoni.

Kwa mujibu wa waraka wa elimu namba 3 wa mwaka 2016 kifungu namba 3.10 (iii) kinaeleza wazi wajibu wa mzazi kushirikiana na uongozi wa shule kuweka utaratibu wa kutoa chakula cha mchana kwa wanafunzi wa shule za kutwa na bweni kulingana na mazingira yao.

Akizungumza na jambo fm afisa elimu mkoa wa Simiyu Khalifa Shemahonge amesema kuwa bado mwamko kwa wazazi katika kuchangia chakula kwa Watoto wao uko chini licha ya wananchi wa mkoa huu kujikita katika kilimo.

“ukiangalia katika wanafunzi 654,000 wa shule za msingi mkoa mzima ni sailimia 56 pekee ndiyo wanaopata chakula kwa mwaka hivyo asilimia 44 watoto hawapati chakula wakati jamii ingekubali kujitoa tungekuwa na akiba ya chakula cha Watoto kwa mwaka mzima kwa sababu shughuli zetu kubwa ni kilimo na ufugaji”afisa elimu Shemahonge.

Elizabeth Philemon mkazi wa Bariadi anasema kuwa kiburi na mazoea baina ya wazazi ndiyo inayorudisha nyuma jitihada hizi huku akihusisha Imani ya wazazi kufikiri kwamba anapochangia chakula anayefaidika ni mwalimu awapo shuleni.

“wewe mzazi huwezi kukaa kuanzia asubuhi hadi saa nane mchana bila kula vipi kuhusu mtoto anaweza kuvumilia? Wazazi wengine ni viburi tu si kwamba hawana michango wanafikiri kwamba tukitoa watakula walimu kumbe tunawatesa Watoto wetu” – Elizabeth.

Pamoja na serikali ya awamu ya sita kufanya ukarabati sambamba kujenga miundombinu ya elimu na kutilia mkazo suala la elimu bila malipo bado ugumu wa Maisha unatajwa kuwa kikwazo kwa wananchi wa mkoa huu na kurudisha nyuma jitihada za kutoa michango shuleni

Mmoja wazazi Simon Kilulu fundi cherehani mjini Bariadi amesema kuwa ugumu wa Maisha bado uko ndani ya familia nyingi kwani kuna wakati unafika hata mlo wa siku kwa familia unakosekana unawezaje kupeleka shuleni.

“hali ni ngumu chakula kupata kwa siku ni shida Watoto utawalisha nini ,tunashinda na njaa siku zingine sasa unaweza kupata chakula cha kupeleka shuleni ,bado tuna  hali ngumu sana sisi wazazi” Mzee Kilulu.

Sambamba na hilo Shemahonge amewahimiza wazazi kutilia mkazo suala elimu ya awali ili kila mwanafunzi anayeandikishwa darasa la kwanza afike akiwa tayari anajua kkk(3) yaani kusoma kuhesabu na kuandika ili kumrahisishia kazi mwalimu wa darasa la kwanza na kupunguza Watoto watakao feli darasa la nne.

“mtoto aliyesoma elimu ya awali hawezi kuwa sawa na mtoto ambaye hajasoma awali tunampa kazi ya ziada mwalimu wa darasa la kwanza ambaye anawanafunza zaidi ya mia moja darasani amuangalie huyu ambaye hakupita awali hapo tutakuwa tunaongeza tu Watoto watakaofeli darasa la nne” Shemahonge.

Nao baadhi ya wazazi wamesema kuwa kumekuwa na shule nyingi za awali mtaani ambazo ufundishwaji wake haukidhi vigezo ambazo kulingana na urahisi mzazi anampeleka mtoto bila kuwa na muda wa ziada wa  kufuatilia maendeleo yake na mwaka unaofuata anampeleka darasa la kwanza kumbe mtoto anakuwa bado hajatimiza vigezo vya kielimu kujiunga na darasa la kwanza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *