Katika hali ya kusikitisha mwanaume mmoja aliyefahamika kwa jina la Magoke Beatus mkazi wa mtaa Wa Elimu Kata Ya Nyankumbu Halmashauri Ya Mji Wa Geita Wilaya Na Mkoa Wa Geita amekutwa amefariki ndani kwake huku mwili wake ukiwa unatoa harufu mbaya.
Wakizungumza na Jambo Fm baadhi ya wapangaji wenzake wakiwemo ndugu wamesema marehemu hakuonekana kwa zaidi ya siku tatu na baadaye walipotafuta chanzo cha harufu hiyo ndipo wakamkuta ndani amefariki huku chanzo cha kifo hicho kikidhaniwa ni unywaji wa pombe za kienyeji kupita kiasi.
Kwa upande wake mwenyekiti wa mtaa wa Elimu Hassan Malima amesema taarifa za tukio hilo alizipata kutoka kwa ndugu wa marehemu na mara baada ya kupata taarifa hizo akatoa taarifa katika kituo cha polisi huku akisema kwa kipindi cha miezi miwili yameripotiwa matukio ya wanaume wawili kufariki wakiwa peke yao na kuwataka wakazi wa mtaa huo kukaa na wenza wao ama ndugu ili wanapopata changamoto waweze kupata msaada wa haraka kuokoa maisha yao.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo kaimu kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Geita Acp Adam Maro amesema marehemu alifariki kwa kukosa hewa ndani ya chumba chake.