Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Askofu Fredrick Shoo ametoa wito kwa Viongozi wa dini zote na Wanasiasa kutokuwagawa Wananchi kwa misingi ya dini au itikadi za kisiasa pamoja na maslahi binafsi.
Akizungumza mkoani Arusha katika maadhimisho ya miaka 60 ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Dkt. Shoo ameiomba Serikali kukemea kwa nguvu zote wale wote wanaoonesha dalili za kuwagawa Wananchi.
“Umoja wa Taifa letu la Tanzania, mshikamano ni muhimu kuliko mtu au kundi lolote. Niwaombe Viongozi wenzangu wa dini zote, niwaombe Wanasiasa waache kabisa kujaribu kuwagawa watu kwa misingi ya dini au kwa misingi ya itikadi yoyote ya kisiasa na kwa misingi ya maslahi binafsi….,”
“Niiombe Serikali yako kukataa na kukemea kwa nguvu zote wale wate wanaoonesha dalili za kutugawa kwa utofauti wa dini zetu hata pale mtu anaposema jambo la kuipendeza Serikali, iwapo amejenga hoja yake katika msingi wa kutugawa kidini au kwa sababu nyingine yoyote huyo akemewe….. Tumkatae hana nia njema.” Amesema Dkt. Shoo.