HOSPITALI YA NDOLAGE  YAZINDUA VIFAA TIBA VYA KISASA VYA HUDUMA ZA KIBINGWA

Hospitali ya Ndolage Mkoani Kagera inayomilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Dayosisi ya Kaskazini Magharibi imeanzisha rasmi huduma za vipimo vya uchunguzi kupitia vifaa tiba vya kisasa.

Vifaa tiba hivyo vya kisasa ambavyo ni CT-Scan, Digital Mammography, Digital X-Ray na Digital Utra- Sound mashine vyenye thamani ya shilingi bilioni 3.3 vimezinduliwa rasmi na Mkuu wa Mkoa wa Kagera Hajjat Fatma Mwassa Mei 17, 2025.

Mwassa alimpongeza Askofu Dkt. Abedinego Keshomshahara  wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Dayosis ya Kaskazini Magharibi kwa uamuzi wake wa kuwekeza katika huduma za afya za kisasa katika Hospitali ya Ndolage ili kuwahudumia wananchi wa Mkoa wa Kagera  mikoa ya jirani na nchi jirani.

“Uwekezaji wa vifaa tiba hivi vya kisasa kwenye sekta ya afya katika Hospitali ya Ndolage ni ishara nzuri ya ushirikiano kati ya Kanisa na Serikali za kufikisha huduma bora za jamii kwa wananchi wake ili wawe na afya imara na bora.” Aliongeza Mkuu wa Mkoa Mwassa

Pia katika hafla hiyo RC Mwassa aliwahakikishia viongozi wa dini na kiroho mkoani Kagera kuwa wapo salama na waendelee na shughuli zao bila wasiwasi kwani Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ipo kazini kuhakikisha usalama wao.

Naye Askofu Dkt. Keshomshahara aliishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ishirikiano na Kanisa hususani kuimarisha mtandao wa umeme kuelekea katika Hospitali ya Ndolage, ikiwa ni pamoja na Taasisi ya Jakaya Kikwete ya magonjwa ya moyo kukubali kushirikiana na Hospitali ya Ndolage kuwahudumia wananchi kupitia vifaa tiba vya kisasa.

Ikumbukwe kuwa vifaa tiba vya kisasa vilivyozinduliwa katika Hospitali ya Ndolage ni pamoja na Digital Mammography na Ocular Utra- Sound mashine vitasaidia kufanya ichunguzi wa haraka wa magonjwa kama Kansa ya matiti na kusaidia upimaji wa magonjwa ya macho, huduma ambazo zilikuwa zinapatikana nje ya mkoa wa Kagera.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *