JAMII IJENGE UTAMADUNI WA KUPANGILIA MUDA – SR. MKOSAMALI

Na Pascal Tuliano – Tabora.

Jamii imeaswa kujenga mazoea ya kupangilia muda (Time management) katika utekelezaji wa majukumu yao ya Kila siku na kuachana na mtindo wa kuishi kiholela.

Rai hiyo imetolewa na Sr. Grace Mkosamali ambaye ni Mwanasaikolojia, mshauri na mkufunzi katika chuo kikuu kishiriki Cha Askofu Mkuu Mihayo Tabora AMUCTA wakati akizungunza katika mahojiano maalum na Radio Jambo Fm ofisini kwake.

Sr. Grace amesema jamii imezoea kuishi katika utaratibu usiofaa wa kutopangilia muda katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

“Watu wengi wamezoea kupanga kitu cha kufanya badala ya kufanya kitu walichopanga. Kila mtu lazima ajue ratiba yake Kila anapoamka, kuishi kiholela sio ustaarabu. Unapaswa ujue unaamka saa ngapi na utafanya jambo gani katika wakati gani.”

Sr. Grace ameongeza kuwa kuishi kwa kuzingatia mpangilio wa muda (Time management) husaidia kuongeza ufanisi wa kazi na huepusha kufanya mambo yasiyo na umuhimu.

Utunzaji wa muda ni changamoto kubwa kwa vijana barani Afrika, hasa kwa wanafunzi wa vyuo vikuu na vijana wanaoanza kazi, pamoja na maisha ya kawaida ndani ya jamii.

Tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa usimamizi mzuri wa muda una uhusiano wa moja kwa moja na mafanikio ya kitaaluma na ustawi wa jumla kwa vijana.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *