Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga amesema Serikali inaendelea kutekeleza mradi wa kupeleka umeme kwenye maeneo ya kimkakati nchini ikiwemo maeneo ya migodi midogo, maeneo ya uvuvi, Viwanda na yanayochagiza shughuli za kiuchumi.
Kapinga ameyasema hayo leo Mei 14, 2025 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la la Mbunge wa Mwibara, Charles Kaijage aliyetaka kufahamu mkakati wa Serikali kuyapelekea umeme maeneo ya uvuvi ili kukuza uchumi wa wananchi wa maeneo hayo.
“Mheshimiwa Naibu Spika Mradi huu wa kupeleka umeme maeneo ya kimkakati umefikia zaidi ya maeneo 300 ikiwemo vituo vya afya na visima vya maji kwa maeneo ambayo yanatoa huduma za kijamii.” Amesema Kapinga.

Akijibu swali la Mbunge wa Igunga, Nicholas Ngassa aliyeuliza lini Serikali itaanza usambazaji umeme kwenye Vitongoji vya Jimbo la Igunga, Kapinga amesema Jimbo la Igunga lina jumla ya Vitongoji 337 ambapo kati ya hivyo, Vitongoji 95 vimepatiwa umeme.
Ameongeza kuwa, katika Vitongoji 15 Wakandarasi wanaendelea na utekelezaji wa miradi kupitia Mradi wa Kupeleka Umeme Vitongojini Awamu ya Pili A (HEP IIA) na Vitongoji 69 zabuni imetangazwa kupitia Mradi wa Kupeleka Umeme Vitongojini Awamu ya Pili B (HEP IIB).
Amesema kuwa, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) itaendelea kutenga fedha za kuvipelekea umeme vitongoji 158 vilivyosalia.
Amesisitiza kuwa, gharama ya kuunganisha umeme kwa maeneo ya Vijijini ni shilingi 27,000/- na kuongeza kuwa, kuna mradi utakaoanza hivi karibuni unaohusisha Vitongoji ambavyo havina laini kubwa ya umeme na vilivyo na kwenye laini kubwa ya umeme.