SERIKALI ITAENDELEA KUIAMINI, KUIUNGA MKONO RED CROSS – DKT. BITEKO

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amesema Serikali itaendelea kuiamini na kukiunga Mkono Chama cha Msalaba mwekundu (RED CROSS) ili kiendelee kufanya kazi yake nzuri ya kuwahudumia Watanzania. 

Dkt. Biteko Amesema hayo Mei 10, 2025 Jijini Dodoma wakati akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika maadhimisho ya miaka 63 ya Chama cha Msalaba Mwekundu (RED CROSS).

Amewahimiza viongozi na wanachama wa chama hicho kutembea kifua mbele na kijisimamia na kujipambanua kutokana na kazi nzuri wanayoifanya bila kujali hali wala mazingira ya kazi husika.

Amesema Serikali tayari kuendelea kufanya kazi na Chama cha Msalaba mwekundu ili kuhakikisha Watanzania wanaendelea kupata huduma bora ikiwemo masuala ya uokoaji maisha.

“Serikali inatambua kazi inayofanywa na Chama cha Msalaba mwekundu kupitia Ofisi na matawi yake nchi nzima,” amesema Dkt. Biteko.”

Amesema kazi zinazofanywa na Chama cha Msalaba mwekundu katika masuala ya kibinadamu zinaonekana ikiwemo ujenzi wa Nyumba 35 kwa ajili ya waathirika wa mafuriko yaliyoikumba Hanang mwaka 2023.
Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Ridhiwani Kikwete amewapongeza Red Cross kwa kazi nzuri ya utoaji wa huduma zinazothibitika kwa vitendo.

Amesema utendaji wao unaonesha na kufuata maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhamasisha utoaji huduma bora kwa Watanzania.

Naibu Waziri wa Uchukuzi ambaye pia ni Rais wa RED CROSS, David Kihenzile amepongeza juhudu za Serikali ya Muungano wa Tanzania katika kuuga mkono juhudi za chama cha Msalaba mwekundu katika utoaji wa huduma kwa jamii.

Pia ameishukuru Serikali kwa hatua yake kuongeza huduma kwa jamii ikiwemo utoaji wa dawa na Vifaa tiba hatua ambayo imeendelea kuboresha maisha ya Watanzania.

Amesema kwa sasa asilimia 30 ya watu wanaopata ajali ndio wanaopata huduma ya kwanza kutokana na wengi kukosa elimu ya utoaji wa huduma hiyo.

Kihenzile pia ametumia jukwaa hilo kuhimiza jamii kujenga moyo wa huruma na upendo na kuwajali wenye shidamiongoni mwa wanajamii ili kujenga taifa lenye maendeleo na ustawi endelevu.

Amesema RED CROSS itaendelea kuungana na Serikali kutoa huduma kwa Wananchi watakaopata majanga ma mahitaji ya aina mbalimbali yanayoweza kutatuliwa kwa msaada wa kibinadamu..

Kaulimbiu ya maadhimisho ya miaka 63 ya Red Cross mwaka 2025 ni Kudumisha Ubinadamu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *