WATOTO WAWILI WAFA MAJI WAKIJARIBU KUVUKA KORONGO

Watoto wawili wa Familia mbili tofauti za Mtaa wa Kibirizi uliopo Manispaa ya Kigoma ujiji, wamefariki Dunia baada ya kusombwa na maji wakati wakipita eneo lisilo na kivuko kwenye korongo liliyopo mtaa huo wakitokea dukani.

Wakizungumza na Jambo FM, wazazi wa watoto hao Mahamudu Musa na Yahaya Juma wamesema mvua kubwa iliyonyesha Jumamosi April 19, 2025 ilisababisha maporomoko ya maji na umauti kwa watoto hao Husein Yahaya (3) na Daud Mahamudu (7).

“Watoto wetu walikuwa ni marafiki mmoja akiwa na hata shl Mia lazima amtafute mwenzake ili waende Dukani wakanunue chochote wanachotaka na ndicho kilichofanyika siku ya tukio walichukuana Kwenda dukani kununu Magolori ya kuchezea kabla mvua haijaanza na ilipoanza iliwakuta hukohuko Dukani,” alisema Yahaya Juma.

Amesema, kijana mmoja ambaye hakufahamika Jina lake alishuhudia tukio hilo na kuanza kuita watu kwa ajili ya msaada wa uokozi lakini hawakufanikiwa zaidi ya kuipata miili yao hao katika eneo la mwa wa ziwa Tanganyika ikiwa ni umbali wa zaidi ya Mita 500 toka eneo la tukio.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kigoma, ACP Philemo Makungu amethibitisha kutokea kwa tukio hilo huku
Wazazi wakisema siyo mara ya kwanza watu kufariki na kujeruhiwa katika vivuko hivyo na kuiomna Serikali kuchukua hatua za haraka kutengeneza vivuko imara.

“Mwaka jana Kuna mama mmoja alikuwa akijaribu kuvuka eneo hilo hilo na alikuwa na mtoto mgongoni aliteleza na mtoto akamponyoka akaenda na maji lakini pia Kuna Baba mmoja yeye aliteleza akavunjika mbavu na yeye hakupo alikufa” alisema Mahamudu Musa.

Katika mazungumzo yake na Jambo Fm Kiongozi wa serikali ya Mtaa wa Kibirizi Kudra Mbonye kuhusiana na juhudi za kukabiliana na changamoto ya vivuko katika mtaa huo anasema walishapeleka maombi TARURA Wilaya ya Kigoma ya kuomba kutengenezewa vivuko hivyo.

“Kama ofisi changamoto ya vivuko katika mtaa wetu tunaijua ipo kutokana na makorongo mbalimbali yaliyopo ni kweli tunahitaji msaada wa haraka kutoka Serikalini kwani yamekuwa ni tatizo kubwa hata kuwavusha wagonjwa kwenda sehemu za huduma hata kina mama wajawazito,” alisema Mbonye.

Pamoja na athari ya Vifo vya watoto hao Mvua hiyo imesababisha zaidi ya Kaya 60 kukosa mahali pa kuishi na mali zao kusombwa na maji katika mtaa wa Mwanga Sokoni na Katubuka Manispaa ya Kigoma Ujiji.

Katika tathimini ya athari za mvua hiyo Katibu Tawala Wilaya ya Kigoma Mjini Mganwa Nzota amesema kati ya Kaya hizo Kaya sita zenye wanakaya 17 zimepata hifadhi ya dharula katika shule ya msingi.

Majengo, Kaya mbili zikipata hifadhi maeneo ya uwanja wa Ndege na wengine wamehifadhiwa na ndugu Jamaa na marafikiAidha katika salaam zake kwa waathirika wa Mvua hiyo.

Mkuu wa wilaya ya Kigoma, Dkt. Rashidi Chuachua amesema katika kutafuta suluhu ya muda mrefu wamewasilisha andiko katika wizara ya (TAMISEMI) kupitia wakala wa Barabara Mijini na vijijini (TARURA) ili eneo hilo liwekwe katika miradi ya uboreshaji wa miji (TACTICS) kwa lengo la kudhibiti athari hizo huku akiwataka wazazi na walezi kuwa makini katika malezi ya watoto hususani katika kipindi hiki cha mvua.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *