Na Eunice Kanumba – Shinyanga.
Waandishi wa habari wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga kupitia Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa (Shinyanga Press Club – SPC) wametembelea bustani ya wanyama ya Jambo Zoo iliyopo katika eneo la Ibadakuli, Mjini Shinyanga, inayomilikiwa na Kampuni ya Jambo Group.
Ziara hiyo imefanyika leo Aprili 19, 2025 ikiwa ni sehemu ya kampeni ya kuhamasisha utalii wa ndani pamoja na kuwaunga mkono wawekezaji wazawa, ambapo imeratibiwa na Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Shinyanga.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mhifadhi wa Jambo Zoo, Babuu Burhan Kajuna, alisema bustani hiyo ina wanyama wa aina mbalimbali ambao wamepewa mafunzo na kuzoea binadamu, hivyo kuwawezesha wageni kupiga nao picha kwa ukaribu.
“Tunawashukuru waandishi wa habari kwa kutembelea Jambo Zoo. Tunawakaribisha wananchi wote waje kufanya utalii wa ndani hapa Shinyanga. Bei zetu ni rafiki kabisa – watu wazima ni shilingi 20,000= na watoto shilingi 10,000/=,” amesema Kajuna.

Ameongeza kuwa wageni wanaofika katika bustani hiyo hupata fursa ya kujifunza kuhusu tabia za wanyama, kupiga nao picha kwa ukaribu, na kuwalisha chakula kwa mikono yao.
Kwa upande wake, Msimamizi wa Chapa kutoka Jambo Group, Nickson George amewataka wananchi kuitembelea bustani hiyo hasa katika kipindi hiki cha sikukuu ya Pasaka, wakiwa na familia zao, huku wakifurahia vinywaji vipya vya Jambo Lemon Lime na Jambo Power Boom.

Aidha, Mratibu wa ziara hiyo, Marco Maduhu ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Tendaji ya SPC ameipongeza Kampuni ya Jambo Group kwa uwekezaji wa bustani hiyo ya wanyama, akisema umeunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan za kuhamasisha utalii wa kupitia filamu ya The Royal Tour.
Bustani ya Jambo Zoo inaendelea kuwa kivutio kikuu kwa wakazi wa Shinyanga na wageni, ikiwa ni sehemu ya utalii wa elimu, burudani na uhifadhi wa wanyama katika mazingira salama na rafiki kwa familia.
