BENKI YA USHIRIKA KUANZISHWA NI MSUKUMO WA WAZIRI MKUU – BASHE.

Waziri wa Kilimo Hussein Bashe ameliambia Bunge la Tanzania kuwa msukumo na ufuatiliaji mzuri wa Waziri Mkuu wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa kwenye sekta ya ushirika nchini pamoja na usimamizi mzuri wa shughuli za Serikali, umewezesha nchi kwa mara ya kwanza kuwa na Benki ya Taifa ya Ushirika kwaajili ya wakulima.

Waziri Bashe ameeleza hayo leo Jumanne Aprili 15, 2025 wakati akitoa maelezo ya hoja mbalimbali zilizowasilishwa wakati wa Mjadala wa hotuba ya bajeti ya Waziri Mkuu kwa mwaka 2025/26 akieleza kuwa Benki hiyo itakayokuwa na matawi manne yatakayokuwa kwenye Mikoa ya Kilimanjaro, Mtwara na Tabora itazinduliwa Aprili 28 na Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Kulingana na Waziri Bashe, Makao makuu ya Benki hiyo yatakuwa Jijini Dodoma, huku Benki hiyo ikiwa tayari imejikusanyia mtaji wa Takribani Bilioni 55 zilizotolewa na serikali kwaajili ya kuwa kama kianzio katika utoaji wa huduma za kifedha kwa wakulima.

Kulingana na Waziri Bashe ukuaji wa sekta ya kilimo kwa mwaka 2021 wakati Rais Samia anaingia madarakani ulikuwa asilimia 2.7 na bajeti ikiwa ikiwa Milioni 290 na kufikia 2024, ukuaji wa sekta hiyo umefikia asilimia 4.2 kukishuhudiwa pia ongezeko la bajeti kutoka Milioni 290 mwaka 2021 hadi kufikia Shilingi Trilioni 1.2.

Waziri Bashe pia ameliambia bunge kuwa mauzo ya nje kwenye sekta ya mazao ya kilimo chini ya maelekezo ya Rais Samia na ufuatiliaji mkubwa wa Waziri Mkuu Majaliwa, yamekuwa kufikia Dola za Marekani Bilioni 3.5 kutoka Dola za Marekani Bilioni 1.2 zilizokuwepo mwaka 2021.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *