Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimesema hakitashiriki, hakijatuma au kuidhinisha mwakilishi yeyote kuhudhuria kikao kilichopangwa kufanyika Aprili 12, 2025 jijini Dodoma, kwa ajili ya kusaini Maadili ya Uchaguzi wa mwaka 2025.
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa CHADEMA, Brenda Rupia imerejelea msisitizo na rejea ya tamko la Katibu Mkuu wa Chama hicho, John Mnyika alilolitoa kupitia ukurasa wake rasmi wa X kusisitiza juu ya azma yake hiyo.

Kwa mujibu wa kanuni za Maadili ya Uchaguzi ni Katibu Mkuu ndiye mwenye mamlaka halali ya kusaini maadili hayo kwa niaba ya chama cha siasa na msimamo huo umetokana na kutokuwepo kwa majibu ya maandishi kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kuhusu barua rasmi iliyowasilishwa na Katibu Mkuu Desemba 29, 2024 akieleza mapendekezo na madai ya msingi ya CHADEMA kuhusu mabadiliko ya mfumo
wa uchaguzi.
Itakumbukwa kuwa, CHADEMA ilishapitisha maamuzi ya yanayojulikana kama:
“No Reforms, No Election” (Bila Mabadiliko, Hakuna Uchaguzi), ambayo yanasimamia hitaji la kufanyika kwa mageuzi ya msingi ya mfumo wa uchaguzi kabla ya kushiriki katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
