KESI YA LISSU YAHAIRISHWA MPAKA APRI 24, AKOSA DHAMANA APELEKWA MAHABUSU.

Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu amesomewa mashtaka manne ikiwemo la uhaini katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya mahakimu wawili tofauti.

Katika kesi hizo mbili zote zimeahirishwa hadi Aprili 24, 2025 huku Lissu akikosa dhamana katika shtaka la uhaini kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na mamlaka ya kuisikiliza.

Lissu alifikishwa mahakamani hapo saa 10: 15 jioni ambapo alisomewa shtaka la uhaini na Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Franko Kiswaga.

Katika shtaka hilo anadaiwa kuwa April 3, 2025 katika Mkoa na Jiji la Dar es Salaam na akiwa Raia wa Tanzania alitengeneza nia ya kuchochea Uma kuzuia uchaguzi Mkuu wa Mwaka huu.

Katika mashtaka matatu ya kuchapisha taarifa za uongo kwenye mitandao ya kijamii alisomewa na Wakili Lukos Harrson mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Geoffrey Mhini.

Katika kesi hiyo ya mashtaka matatu, Lissu alikana makosa yote matatu ambapo alipewa masharti ya dhamana ya mdhamini atakayesaini bondi ya Shilingi Milioni Tano, ambapo baada ya kutimiza masharti hayo kesi imeahirishwa hadi Aprili 24, 2025.

Katika mashtaka hayo matatu ya kuchapisha taarifa za uongo,inadaiwa kuwa April 3 ya mwaka huu katika Mkoa na Jiji la Dar es Salaama Mshtakiwa alichapisha taarifa za Uongo kwenye mtandao wa Youtube zikisema kuwa Katika uchaguzi wa serikali za Mitaa wa mwaka 2024 wagombea wote wa CHADEMA walienguliwa kwa maelekezo ya Rais huku akijua ni uongo.

Katika shtaka la pili ni Kuchapisha taarifa za uongo kwenye mtandao wa Youtube zilisema kuwa Polisi wa nchi hii wanatumika kuiba kura huku akijua kuwa ni uongo.

Na katika shtaka la tatu inadaiwa kuwa April 3 mwaka huu mkoa na Jijini Dar es salaam mshtakiwa alichapisha taarifa kwenye mtandao wa Youtube zikisema kuwa Majaji wa nchi hii ni CCM na hawawezi kutenda haki kwa kuwa wanapenda kuteuliwa kuwa majaji wa mahakama ya Rufaani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *