Katika katika kuboresha utoaji wa huduma kwa Watu Wenye Ulemavu Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kuhakikisha jamii ya Watu Wenye Ulemavu inaishi katika mazingira salama na kushiriki katika shughuli za kijamii, kisiasa na kiuchumi.
Kauli hiyo imetolewa hii leo Bungeni jijini Dodoma na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ambaye pia amesema Serikali imezindua Mpangokazi wa Taifa wa Ustawi na Haki kwa Watu Wenye Ualbino.
“Waheshimiwa Wabunge kama mnavyofahamu, Serikali imezindua Mpangokazi wa Taifa wa Ustawi na Haki kwa Watu Wenye Ualbino kwa Mwaka 2024/2025 2028/2029,” amefafanua Waziri Mkuu.

Aidha, amesema mpangokazi huo, unaainisha hatua zinazohitajika katika kuzuia, kukabiliana na kutokomeza ukatili kwa Watu Wenye Ualbino.
Katika hatua nyingine Majaliwa amesema, “kwa upande wa maendeleo ya vijana, serikali imeendelea kuweka mazingira rafiki ili waweze kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo, kujipatia ajira na kujikwamua kiuchumi.
Katika mwaka 2024/2025 serikali imezindua Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana ya mwaka 2007, Toleo la 2024 pamoja na mkakati wake. Sera hiyo imezingatia mazingira na mahitaji ya vijana ikiwemo elimu na ujuzi kwa vijana; uvumbuzi na ubunifu kwa vijana; vijana na mapinduzi ya kidijitali; ajira kwa vijana; na ushiriki wa vijana katika sekta za kijamii na kiuchumi.”
“Kwa mwaka 2025/2026, Serikali itatekeleza programu za stadi za maisha, malezi na makuzi na uratibu wa maendeleo ya vijana; na kuendelea kuhamasisha vijana kushiriki kikamilifu katika shughuli mbalimbali za kiuchumi ili kuweza kujipatia ajira na kuinua kipato chao,” alibaijisha Waziri Mkuu.