KARUME DAY: HATUA MUHIMU ZA KUKUMBUKWA MAISHANI

Rais wa kwanza wa Zanzibar, hayati Abeid Amani Karume ni mmoja wa waasisi taifa, aliongoza Zanzibar baada ya mapinduzi yaliyomuangusha Sultani aliyekuwa akitawala visiwa hivyo.

Mwaka 1964 mwanzoni baada ya mapinduzi hayo Zanzibar iliungana na Tanganyika iliyokuwa inaongozwa na mwalimu Julius Nyerere na kuzaliwa Tanzania.

Karume alipatwa na umauti baada ya kupigwa risasi visiwani humo April 7, 1972  akiwa na miaka 67, katika ofisi za makao makuu ya CCM eneo la Kisiwandui visiwani Zanzibar.

Historia inaeleza kuwa alipigwa risasi wakati akicheza mchezo wa bao na wenzake, ambapo aliyemuua naye aliuawa papo hapo na walinzi wa Karume, baada ya kutokea kwa tukio hilo.

Hata hivyo Mzee Karume alikuwa makamu wa Rais wa kwanza wa Jamuhuri ya muungano wa Tanzania na Mwalimu Nyerere ndiye aliyekuwa Rais ambapo Karume alitawala Zanzibar kwa miaka minne.

Sheikh Abeid Aman Karume alizaliwa katika mji wa Pongwe kisiwani Unguja Agosti 4, 1905 akitokea katika familia ya watu 6 ambapo baba yake aliaga Dunia mwaka 1909 wakati Abeid akiwa na umri wa miaka minne.

Alipata elimu ya Qur’an na kuanza masomo yake ya kimsingi katika shule ya Mwera, mwaka 1913 kisha alihamia kwa mama yake  mji wa Unguja kuendelea na masomo yake na  huko aliishi na baba yake mdogo aliyekuwa Sajin katika jeshi la Polisi la Mfalme.

Mwaka wa 1920 alifanya kazi kama Baharia katika boti za usafirishaji wa mizigo na hatimaye alipata cheo cha Kamanda wa Wafanyakazi na baada ya  mwaka wa 1938 aliongoza kundi la boti za mvuke zilizobeba abiria bandarini.

Aliondoka Zanzibar katika miaka ya mwanzo ya maisha yake, akihamahama sehemu mbalimbali za dunia hadi alipofika London, ambapo alipata uzoefu mkubwa katika jiografia ya kisiasa na masuala ya Kimataifa wakati wa mikutano yake na wasomi Waafrika q Kamuzu Banda wa Malawi.

Karume alijiingiza katika siasa kwa mara ya kwanza mwaka 1954, na kabla ya Mapinduzi ya 1964, Karume aliongoza Chama cha Afro-Shirazi kupinga muungano wa utawala wa Kiarabu ulioonekana kuwa na lengo la kudumisha utawala wa kisiasa na kiuchumi wa jamii ya Kiarabu.

Januari 12, 1964, wafuasi wa chama cha Afro-Shirazi walimshinda Sultan Jamshid bin Abdullah na kuanzisha utawala wa Afrika, na Karume alikuwa Kiongozi wa Baraza la Mapinduzi na kisha Rais wa Jamhuri mpya ya Watu wa Zanzibar.

Hapo Sheikh Abeid Karume alipewa jina la Rais wa kwanza wa Zanzibar baada ya mapinduzi yake ya kukomesha ufalme wa Zanzibar, tena kulingana na historia rasmi ya Zanzibar, Abeid Karume alikuwa kiongozi wa Chama cha Afro-Shirazi na ndiye mpangaji na Kiongozi wa mapinduzi.

Hatua yake ya pili muhimu ya kisiasa ni pale  alipokubali kuunda Muungano na Rais wa Tanganyika Julius K. Nyerere Aprili, Muungano ambao ulisababisha nchi mpya ya Tanzania, hivyo akawa Makamu wa kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Aprili 7, 1972 Karume aliuawa na watu wanne wenye silaha katika Makao Makuu ya Chama chake cha Afro-Shirazi.

Hivyo, siku hii inakuja kuadhimisha kumbukumbu yake, ikiwa ni siku maalum kwa watanzania kukumbuka mafanikio yake, ambapo pia Viongozi na Marais wetu husherehekea siku hiyo kwa kwenda kuzuru kaburi na kuweka mashada ya maua juu ya kaburi lake na kufanya Sala ya kumuombea aendelee kupumzika kwa amani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *