Na Adam Msafiri – Mara.
Diwani wa Kata ya Nyamakokoto Wilayani Bunda Mkoani Mara, Emmanuel Mlibwa na wenzake watatu wamefikishwa katika mahakama ya wilaya ya Bunda, wakituhumiwa kwa makosa matano ya uhujumu uchumi.
Aidha katika tuhuma hizo yapo makosa ya kujihusisha na vitendo vya Rushwa kwa kuandaa vikundi hewa ili kujipatia fedha kiasi cha shilingi milioni 3 ambazo ni mkopo wa asilimia 10 zinazotolewa na Serikali kwa vikundi vya Wanawake, Vijana na Watu wenye ulemavu, matumizi mabaya ya madaraka pamoja na kughushi nyaraka.
Kesi hiyo namba 74/41/2025 imesomwa Aprili 4,2025 mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya ya Bunda, Betron Sokanya na mwendesha mashtaka wa TAKUKURU.

Amesema mshtakiwa Mboji William ambaye ni Afisa Maendeleo ya Jamii, Godfrey Merengo(Mjasiriamali), Khalid Kabusule (Mjasiriamali) na Emmanuel Malibwa ambaye ni Diwani wa kata ya Nyamakokoto-Bunda, walitenda makosa hayo kwa nyakati tofauti.
Hata hivyo, watuhumiwa wote wamekana makosa hayo na kesi imeahirishwa hadi Mei 2, 2025 itakaposomwa tena na watuhumiwa wapo nje kwa dhamana.