Fangasi miguuni hujumuisha fangasi katika eneo lolote la mguu na kanyagio kama vile kanyagio na katikati ya vidole.
DALILI.
Dalili kubwa ya fangasi ni muwasho unaokulazimisha kujikuna na kujihisi raha au utulivu unapojikuna, harufu nzito ya kuoza katika miguu hasa uvuapo viatu, kumomonyoka ama kulika kwa ngozi yenye fangasi miguuni. Pia kuvuja kwa majimaji yenye kuteleza na harufu nzito, maumivu au kuhisi kuchomachoma baada ya kuchubuka na pia mara nyingine kuhisi kuwaka moto.

Ugunduzi wa fangasi wa ngozi ya miguu ni rahisi, huhitajiki kwenda maabara, wahudumu wa afya wanaweza kugundua kwa kupata historia ya dalili na kutazama kwa macho. Mara nyingine unaweza usihitaji kupewa dawa za kukabiliana na fangasi wa miguu, elimu ya afya inaweza kukubadili tabia na ukadhibiti fangasi wa ngozi ya miguuni bila dawa japokuwa dawa hasa za poda au cream zipo.
KINGA.
Moja ya njia rahisi za kukabiliana na kujikinga na fangasi ni kubadili mienendo ya kimaisha ikiwamo kupenda kuwa msafi wa kimwili pamoja na kufua nguo zinazovaliwa ikiwamo soksi ambazo wengine huzivaa kwa muda mrefu bila kuzifua.

Tumia soksi zenye asilimia nyingi ya pamba ili kuweza kunyonya jasho la miguuni, kutumia kitambaa safi au taulo dogo kwa ajili ya kukaushia maji baada ya kuoga au unapotoka kazini, matembezini na mchezoni. Mara tu baada ya kutoka katika shughuli zako vua viatu vya kufunika na tumia viatu vya wazi, kausha kwa kitambaa kikavu maeneo ya miguuni katika upenyo wa vidoleni.
MATIBABU.
Matibabu ya dawa za fangasi za kupaka zilizo katika mtindo wa poda zinaweza kutumika kutibu, kwa fangasi sugu, dawa za kumeza zinaweza kutolewa. Kama kukiwa na maambukizi mchanganyiko na bakteria dawa za antibiotic zinaweza kutolewa. Mara nyingine fangasi zinaweza kupata nyufa za vidoleni zikatengeneza vidonda ambavyo vinaweza kupata maambukizi wa bakteria ikiwamo wale wa tetenasi.

Ukiwa una tatizo hili kiasi cha kufikia kupata vidonda miguuni, hakikisha unapata tiba . Fangasi za miguuni ni ugonjwa kama magonjwa mengine, hivyo wanaogua wasipuuze wakidhani ni tatizo dogo, wawahi kupata tiba kwa kuwaona wataalamu wa afya.