JKCI YAPOKEA WAGONJWA 689 WA MATAIFA MBALIMBALI

Na Gideon Gregory – Dodoma. 

Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Kwa kipindi cha miaka minne imepokea wagonjwa 689 kutoka mataifa mbalimbali kuja kupatiwa huduma ya matibabu ya moyo. 

Hayo yameelezwa hii leo Februari 26, 2025 Jijini Dodoma na Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo, Dkt. Peter Kisenge wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio waliyoyapata katika kipindi hicho ambapo ameyataja mataifa hayo kuwa ni Somalia, Kenya, Msumbiji, Nigeria, na hata nchi za Ulaya kama Ujerumani, Ufaransa, na Uingereza. 

“Hii inathibitisha ubora wa huduma zinazotolewa katika taasisi hiyo na jinsi ilivyojijengea heshima kimataifa,” amesema. 

Amesema katika eneo la upasuaji wa moyo, JKCI imefanya upasuaji mkubwa wa kufungua kifua kwa wagonjwa 2,784, ambapo mishipa ya damu, valvu za moyo na mapafu zilibadilishwa au kurekebishwa. Pia, wagonjwa 8,789 walifanyiwa uchunguzi na matibabu ya mishipa ya damu ya moyo kwa kutumia mtambo wa Cathlab, ambao ni maabara maalum ya mionzi.

Ili kuhakikisha kuwa huduma zinaboreshwa zaidi, Serikali ya Awamu ya Sita imewekeza zaidi ya shilingi bilioni 2.16 katika taasisi hiyo na Fedha hizo zimetumika katika upanuzi wa ICU za watoto na watu wazima, ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa, tiba mtandao, na mafunzo kwa wataalamu wa afya.

“Uwekezaji huu umeongeza uwezo wetu wa kuhudumia wagonjwa wengi zaidi na kwa ubora wa hali ya juu,” amesema Dkt. Kisenge.

Ameongeza kuwa katika sekta ya utafiti na mafunzo, JKCI imeingia makubaliano na vyuo vikuu mbalimbali kama Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha New York nchini Marekani, na Chuo Kikuu cha Jagiellonian cha Poland kwa lengo la kuboresha tafiti za magonjwa ya moyo na kutoa mafunzo kwa wataalamu wa afya.

Kuhusu huduma za tiba mkoba zijulikanazo kwa jina la Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services amesema kuwa zimetolewa katika mikoa 20 na maeneo ya kazi 14 kwa watu 21,324 watu wazima wakiwa 20,112 na watoto 1,212 walifanyiwa uchunguzi wa magonjwa ya moyo.

Dkt. Kisenge amefafanua kuwa kati ya hao 8,873 watu wazima wakiwa 8,380 na watoto 493 walikutwa na matatizo mbalimbali ya moyo na kuanzishiwa matibabu. Wagonjwa 3,249 watu wazima 2,765 na watoto 484 walikutwa na matatizo yaliyohitaji matibabu ya kibingwa na kupewa rufaa ya kuja kutibiwa katika Taasisi yetu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *