Mtu mmoja, Abdallah Mohammed (40), fundi friji na mkazi wa Mataya, Kata ya Kiromo, Wilaya ya Bagamoyo, anatafutwa na Jeshi la Polisi Mkoani Pwani, kwa tuhuma za mauaji ya mzazi mwenzie, Naomi Mwakajengele ‘Anangisye’ (28).
Taarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoani Pwani, Salim Morcase imeeleza kuwa tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia Februari 11, 2025 ambapo wawili hao walikuwa chumbani na ndipo zikasiskika kelele za kilio cha Naomi akidai mwenza wake anamuua.
Amesema, uchunguzi wa awali umebaini kuwa mwili wa marehemu Naomi ambaye alikuwa ni Mwalimu wa Shule ya Msingi Mataya, umechomwa na kitu chenye ncha kali kwenye maeneo ya ubavu wa kulia, ubavu wa kushoto na kwenye chembe ya moyo.
![](https://jambofm.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/01JE9612DEQZQW2YJZMD9SMGY5.jpg)
“Baada ya kelele hizo, Abdallah Mohammed alitoka chumbani na akaenda kwa dada wa kazi na kumtaka kulala na watoto wao wawili, mwenye umri wa miaka minne na mwingine wa miaka miwili, ambao awali walikuwa wamelala na mama yao,” imeeleza taarifa hiyo.
Hata hivyo, Kamanda Morcase amebaijisha kuwa majira ya asubuhi, dada wa kazi alishtuka baada ya kuona mlango wa nyumba ukiwa wazi na Abdallah Mohammed akiwa ametoweka kusikojulikana.
“Inavyoonekana, wawili hao walikuwa na migogoro ya muda mrefu, hali iliyopelekea kutokuishi pamoja kwa kipindi fulani kabla ya Abdallah kurejea tena nyumbani kwa Naomi wiki mbili zilizopita, hatimaye, tukio hilo lilitokea,” alisema.